31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

BoT, IFC zatoa elimu mikopo na fedha

  • Taarifa sahihi za mikopo ni muhimu
  • Tumia mkopo kiuwekezaji

GABRIEL MUSHI-DAR ES SALAAM

MKOPO ni nyenzo muhimu ya uchumi kwa kuongeza uwezo wa kupata bidhaa na huduma kwa gharama kupitia mkopo na hivyo kuwasaidia watu kununua vitu ambavyo mtiririko wao wa fedha wa kawaida hauruhusu.

Lakini watu wengi wanaukosea mkopo pale wanapoutumia ili kuishi nje ya uwezo wao wa kipato na bila kuzalisha na hivyo unasababisha machungu kwa fedheha na aibu itokanayo na  ukopaji wa kutowajibika.

Lakini kwa kutumia mikopo vizuri na kujua taarifa zao za mikopo, Watanzania wataweza kupanga mustakabali bora wa maisha kwani ni ukweli usiokataliwa kwamba matumizi bora ya mikopo yana manufaa mengi kwa mkopaji. Ndio maana wabobevu wa uchumi husema; ‘Tumia mkopo kama nyenzo ya kuwekeza katika mustakabali wako, kuliko kama njia ya kuishi maisha

ya anasa katika kipindi kifupi.’

Ili kuepukana na madhila ya namna mbalimbali katika ulimwengu wa sasa ni vema kujua taarifa ya mikopo yako na kuiheshimu.

Taarifa ya mikopo ni waraka ambao unaonyesha taarifa ya ukopaji wa mtu na utaratibu mwenendo wa marejesho. Ukopaji unaweza kuwa mikopo uliyopata au bidhaa au huduma ulizonunua kwa mkopo.

Taarifa ya mikopo inawasaidia wakopeshaji (kama vile benki, makampuni ya simu za mkononi, wafanyabiashara wa samani n.k.)

kutambua uwezekano wa mkopaji kurejesha mkopo au madeni mengine

na kufanya malipo kwa mujibu wa makubaliano.

Kwa mfano, kama unaomba mkopo kwenye benki wa kulipa ada ya shule, benki itatumia taarifa yako ya mikopo ili kuamua kukupa mkopo au lah na kwa masharti yapi (kwa mfano, viwango vya riba au masharti ya marejesho).

Taarifa ya mikopo inaweza pia kuwasaidia wengine (mfano: waajiri, wamiliki wa nyumba na wafanyabiashara) ambao wanataka kuwa na uhusiano na wewe wa kibiashara au vinginevyo kuamua kiwango cha uaminifu, mtizamo na tabia ya kutimiza wajibu wa kifedha.

Katika kuhakikisha Watanzania wanaondokana na matumizi ya anasa ya

mikopo pamoja na kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mikopo na taarifa za mikopo, Benki Kuu ya Tanzania, kwa kushirikiana na Taasisi ya International Finance Corporation ambayo ni mwanachama wa Kundi la Benki ya Dunia, imezindua kampeni ya uelimishaji wa mikopo kwa Watanzania  wote.

Kampeni hiyo ya miezi mitatu inalenga kuongeza uelewa na mwamko

kuhusu taarifa za mikopo na kukuza upatikanaji wa mikopo. Kampeni

ya kuelimisha umma inayosema; “Pata Taarifa Yako ya Mikopo Leo.

Angalia Hali Yako ya Kifedha ili Kupanga Mustakabali Wako Bora wa

Kesho inaungwa mkono na wadau mbalimbali katika sekta ya huduma

za fedha ambao wameahidi kusaidia kusambaza ujumbe kuhusu

umuhimu wa upatikanaji wa mikopo na jinsi Watanzania wanavyoweza

kuishi maisha bora kwa kuweza kupata taarifa za mikopo yao na kujua

historia ya mikopo yao.

Kampeni uelewa mikopo

Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, alisema ili kuwa na mfumo mzuri wa taarifa za mikopo  ni wajibu wa wadau wanne wakubwa ambao ni watoa mikopo, kampuni za kuandaa taarifa za mikopo, wakopaji na mamlaka za udhibiti na usimamizi.

“Elimu kuhusu masuala ya fedha ni muhimu katika mfumo mzima wa taarifa za mikopo.

Kampeni hii ya elimu kwa umma inalenga kuwaelimisha watumiaji wa huduma za fedha na wadau wengine kukuza uelewa wao kuhusu taarifa za mikopo ili kuongeza ushiriki katika matumizi ya taarifa za mikopo hapa nchini,” alisema.

Akifafanua kwa kina kuhusu taarifa za mikopo hiyo, Meneja Msaidizi, Mfumo wa Kumbukumbu za Wakopaji (Credit Reference System) kutoka BoT, Nkanwa Magina, anasema taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo hutoa ‘Alama ya Mikopo’ ambayo ni nambari inayozingatia taarifa na historia ya mikopo yako.

Anasema taarifa ya mikopo na alama ya mikopo ni vitu viwili tofauti kwani taarifa ya mikopo inatoa historia ya kina ya mwenendo wa mikopo yako; kwa mfano, kama unarejesha kwa wakati, kuchelewa kurejesha au kushindwa kulipa mikopo au bidhaa/huduma ulizopata kwa mkopo wakati alama ya mikopo ni daraja unalopewa (rank) likionyesha tathmini ya uwezo wa kurejesha mikopo. Alama hii inazingatia historia ya mikopo yako.

Umuhimu wa usimamizi wa mikopo

Anasema usimamizi mzuri wa mikopo ni muhimu. Historia nzuri ya mikopo ni muhimu kwako kukuwezesha kupata mkopo nafuu, huduma za simu ya mkononi, na hata kazi.

Kuhakiki taarifa yako ya mikopo mara moja kwa mwaka inayopatikana

bila malipo, kutakuletea mafanikio kwa kukuandaa vema utakapoenda kuomba mkopo.

Pia unakusaidia kuweka akiba kwa ajili ya mambo yasiyotarajiwa au ya dharura. Historia nzuri ya mikopo inaweza kukusaidia kustahili viwango vya chini vya riba na ada, hivyo kuondokana na kutenga fedha kwa ajili ya dharura na gharama zisizotarajiwa,” anasema.

Anasema mikopo inasaidia kupata mahitaji ya sasa, kama vile nyumba au ada ya shule ya mtoto wako, kwa kuzingatia ahadi yako ya kulipa kwa awamu na kwa muda uliopangwa.

Pia, inaweza kukusaidia kukuza biashara yako.

Taarifa ya mikopo inaonyesha nini hasa?

Meneja wa IFC – Tanzania, Manuel Moses anasema taarifa ya mikopo

inaonesha taarifa binafsi: utambulisho na taarifa ya mawasiliano na ikiwezekana historia ya ajira; idadi na aina za akaunti za mikopo ulizonazo (mikopo binafsi na ya nyumba, malipo ya maji na umeme, na malipo kupitia simu ya mkononi); ni kiasi gani cha mkopo kilichochukuliwa ukilinganisha na kilichokubaliwa, kiasi cha deni lililobakia na hali ya mikopo yako pamoja na taarifa zilizo wazi kwa

umma kama vile uamuzi wa mahakama dhidi yako unaoathiri uwezo wa

kurejesha mikopo mfano kutangazwa kufilisika, orodha ya makampuni

au watu ambao waliomba nakala ya taarifa yako ya mikopo.

Nani anakusanya na kutoa taarifa za mikopo?

Uandaaji taarifa za mikopo

Taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo zinapata taarifa hizo kutoka kwa wakopeshaji na watoa huduma kama vile benki na taasisi za huduma ndogo za fedha.

Kila mwezi, benki na taasisi zinazosimamiwa na Benki Kuu zinawajibika kuwasilisha taarifa zao za mikopo kwenye taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo.

Meneja Maendeleo ya Biashara kutokaDun & Bradstreet, Josephine

Temu anasema kwa sasa, kuna taasisi mbili zilizopatiwa leseni na Benki

Kuu ya Tanzania kuandaa na kutoa taarifa za mikopo hapa Tanzania

ambazo ni Creditinfo Tanzania Limited na Dun & Bradstreet. Ni taasisi

zinazokusanya na kutunza taarifa za mikopo yako. Taasisi hizo zinatoa

taarifa za mikopo kwa kampuni au watu wanaozihitaji kama vile benki unakoomba mkopo.

Anasema ripoti hiyo ya mikopo unaweza kuipata kwa taasisi hizo

(Creditinfo na Dun & Bradstreet) mara moja kwa mwaka bila malipo ili

kujua hali ya mikopo yako na kupanga mustakabali wako bora wa kesho.

Anasema ili kupata taarifa ya mikopo unatakiwa kuwasilisha nakala ya

kitambulisho chako cha taifa au kingine kama leseni ya udereva, hati ya kusafiria.

“Jaza na wasilisha fomu ya maombi ya taarifa yako ya mikopo katika

taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo ambazo kwa sasa ni Creditinfo au

Dun & Bradstreet,” anasema.

Mambo muhimu ya kuangalia kwenye taarifa ya mikopo

Akifafanua kuhusu mambo hayo, Tonny Missokia anasema kwanza kabisa ni taarifa binafsi kwa kuhakikisha taarifa binafsi kama vile jina,hadhi ya ndoa, anwani, taarifa za ajira na namba za mawasiliano ni sahihi.

Pili, ni historia ya taarifa ya mikopo. Sehemu hii inaonyesha idadi na

aina ya mikopo uliyonayo (kwa mfano, mikopo ya muda mfupi, mikopo

ya nyumba, malipo ya mafaa, malipo kupitia simu ya mkononi).

Hakikisha kuwa mikopo iliyoonyeshwa, kiasi unachodaiwa, na historia yako ya malipo viko sahihi.

Tatu, ni maulizo. Maulizo kwenye taarifa yako ya mikopo hutokea wakati kampuni au taasisi inayotarajia kukupatia mkopo inapokagua ripoti yako ya mikopo na kutumia taarifa hiyo kuamua ama kukupatia mkopo au kutokukupatia mkopo. Kwa mfano, kama unaomba mkopo wa nyumba au gari, kampuni au taasisi inayokupa mkopo itakagua taarifa

yako ya mikopo ili kuisaidia kujua kama unastahili mkopo.

Namna ya kuboresha tathmini ya mkopo

Aidha, Meneja Maendeleo ya Biashara kutoka Creditinfo, Tonny Missokia, anafafanua kwa kina mambo ya kufanya; Lipa ankara zako kwa wakati. Kama una ankara ambayo haijalipwa kwa wakati, fanya utaratibu wa kuilipa.

Ishi kulingana na kipato chako. Kila mpango mzuri wa fedha unaanza na bajeti nzuri. Kama unataka kulipa ankara na kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya mtoto wako, hatua yako ya kwanza katika kuyafanya malengo hayo ni kuwa na bajeti.

Anasema kupanga bajeti kunafanya iwe rahisi kufuatilia na kudhibiti matumizi yako. Pia, kunakusaidia kupanga mipango yako ya fedha ya baadaye.

“Kupanga bajeti kunamaanisha kuweka mpango wa kina unaoonyesha kiasi cha fedha unachozalisha na kiasi unachotumia.

“Japokuwa kupanga bajeti kunaweza kuchosha na kutumia muda mwingi, matokeo yake yana thamani kubwa zaidi.”

Ingawa inaweza kuwa vigumu kuanza kutumia bajeti, baada ya muda mfupi matumizi ya bajeti yatazoeleka na kuwa rahisi. Unaweza hata kushangaa ni kwa kiasi gani umefaidika kutokana na kutumia bajeti, kama vile kujenga uwezo wa kupunguza matumizi au kujiwekea akiba kwa ajili ya matukio maalumu.

Mambo usiyopaswa kufanya:

Kupuuzia hali halisi. Kufanya hivyo ni

kujiongezea matatizo yako.

“Usisubiri mpaka ushindwe kabisa kulipa ankara zako ndipo uzungumze na taasisi iliyokukopesha. Badala yake, zungumza na mkopeshaji mara tu unapokuwa na matatizo ya kifedha ili kupanga utaratibu wa kurejesha mkopo hali yako ya kifedha ikiimarika,” anasema.

Tofauti kati ya deni zuri na deni baya

Anasema uzuri au ubaya wa mkopo utategemea jinsi ulivyopanga na kuutumia. Mkopo mzuri ni ule ambao utakuwezesha kuongeza uwezo wako wa kifedha kadiri siku zinavyoendelea.

Mifano ya deni zuri ni mkopo wa nyumba au mkopo wa mwanafunzi. Faida utakazopata baadae zitakuwa ni thamani ya nyumba au sifa za taaluma na ujuzi.

Anasema mkopo mbaya, kwa kawaida ni ule ambao unatumika kununua vitu ambavyo vinazalisha kidogo au havina thamani yoyote katika kipindi cha muda mrefu.

“Aina mojawapo ya mikopo mibaya ni pale unapokopa fedha ambazo huwezi kuzirejesha.”

Kanuni ya marejesho ni kuwa: Ukishindwa kufanya rejesho hata moja, huo tayari ni mkopo mbaya.

Vitu vinavyonunuliwa kwa kutumia fedha za mkopo mbaya kwa kawaida hupoteza thamani kabla mkopo haujalipwa.

Kwa mfano, kununua vitu vya matumizi ya kila siku ambavyo malipo yake yanafanyika kwa zaidi ya miezi sita, ni njia mbaya ya kutumia mkopo.

Kusahihisha dosari katika taarifa yako ya mikopo

Aidha, Josephine Temu anasema kama kuna dosari kwenye taarifa yako ya mikopo, unapaswa kuwasilisha pingamizi kwa taasisi iliyoandaa taarifa hiyo ili zirekebishwe au zifutwe.

“Unapowasiliana na taasisi husika, unapaswa kutoa maelezo binafsi, kama vile jina lako, anwani, tarehe ya kuzaliwa na kitambulisho; maelezo mahsusi kuhusu taarifa ambazo hukubaliani nazo na msingi wa kutokubali kwako.

“Taasisi iliyoandaa taarifa ya mikopo lazima ichunguze dosari ndani ya siku mbili za kazi. Kama dosari inatokana na taasisi iliyoandaa taarifa ya mikopo, taasisi hiyo inawajibika kutoa majibu ndani ya siku 15 za kazi. Ikiwa dosari zinatokana na taasisi ya mikopo au huduma/bidhaa inayowajibika na suala hilo, itatakiwa kutoa majibu ya pingamizi lililotolewa ndani ya siku 15 za kazi. Pia unastahili kupata nakala ya

taarifa ya mikopo baada ya masahihisho bila malipo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles