Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, ametoa msaada wa taulo za kike kwa shule 10 za sekondari zilizoko katika jimbo hilo kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo wakati wote.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa kampeni aliyoianza ya kugawa taulo hizo ambapo ameweka juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya mbunge huyo ambaye yuko bungeni Dodoma, Katibu wake Lutta Rucharaba, amesema msaada uliokabidhiwa leo kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari Magoza, Kinyerezi, Kinyerezi Mpya na Bonyokwa umetolewa kwa ushirikiano wa Klabu ya Fountain Gate Princess.
Shule nyingine zilizokwishapatiwa msaada huo ni Kiwalani, Ilala, Minazi Mirefu, Majani ya Chai, Kisungu na Ari.
“Mheshimiwa mbunge amedhamiria watoto wa kike wasikose masomo kwa sababu ya taulo za kike, bado shule sita nazo tutazifikia hivyo tunatoa wito kwa wadau wengine mbunge yuko kwenye kampeni muhimu wawiwe kumuunga mkono kusaidia watoto wa kike wasikose masomo,” amesema Rucharaba.
Naye Ofisa Utawala na Fedha wa Klabu ya Fountain Gate Princess, Happy Joshua, amesema waliona wasiishie kusaidia tu wachezaji wao na kuamua kutanua wigo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali na kuahidi kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.
“Tuna wachezaji ambao ni wanafunzi na wamekuwa na changamoto kama hii hivyo tulijaribu kufikiria na wanafunzi wengine,” amesema Happy.
Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake Mwajuma Mkuta anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari Magoza, amesema kukosa vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi kunaathiri mahudhurio ya wanafunzi hivyo msaada huo utasaidia kukuza kiwango cha taaluma.