Na SAMWEL MWANGA
SERIKALI Wilaya ya Maswa imewaonya wamiliki wa pikipiki zinazosafirisha abiria maarufu kwa jina la bodaboda kuhakikisha madereva wanaowakabidhi pikipiki hizo ni wale waliopata mafunzo ya usalama barabarani.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe alipofunga mafunzo ya usalama barabarani yaliyoandaliwa na uongozi wa wilaya kwa waendesha pikipiki za kubeba abiria mjini Maswa.
Aliwataka madereva hao kuheshimu kazi hiyo kwa kuwa inawapatia kipato hivyo kuzingatia sheria za usalama barabarani na siyo vinginevyo.
DC alisema wamiliki wake wanapaswa kutambua kuwa hiyo ni fursa ya uchumi hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanawakabidhi pikipiki watu wenye ujuzi.
“Wamiliki wa bodaboda mnawekeza fedha nyingi katika kununua bodaboda lakini wengi wenu mnawakabidhi madereva ambao hawana mafunzo na wanakuwa chanzo cha ajali za barabarani.
“Hakikisheni wamepewa mafunzo na ambao hawana wasaideni wapate kuepuka kupoteza pikipiki zenu na nguvu kazi ya taifa kwa ajali ambazo siyo za lazima,”alisema.
Alisema lengo la wilaya hiyo kuandaa mafunzo hayo ni kuwafanya waendesha pikipiki hizo wawe salama pamoja na kujali usalama wa watumiaji wengine wa barabara na kuepusha ajali zisizokuwa za lazima na kupata leseni za udereva.
Pia aliwataka madereva hao kuunda vikundi vyao kwa kuwa na Chama cha Bodaboda wilayani humo serikali iweze kuwasaidia kwa kuwapatia mikopo waweze kwa siku za baadaye kumiliki pikipiki zao binafsi na hata bajaj na Hiace.
“Undeni vikundi ambavyo mtavisajili na serikali itawasaidia kupata mikopo muweze kujitegemea maana waendesha bodaboda mlio wengi hizo pikipiki mnazofanyia kazi ya kubeba abiria si zenu.
“Hivyo ni vizuri kila mmoja akawa anamiliki pikipiki yake hata ikibidi muweze kumiliki bajaji na hata Hiace,”alisema.
Mkuu wa Usalama Barabara Wilaya ya Maswa, Bwire Essore alisema ajali nyingi zinazotokea barabara na kusababisha watu wengi kufariki dunia na kupata vilema.
Alisema nyingi zinasababishwa na waendesha bodaboda wengi ambao hawana mafunzo ya usalama barabarani.