26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MNH YAELEZA SABABU ZA KUFURIKA WODI YA WAZAZI

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeeleza sababu za kuwapo msongamano katika wodi ya wazazi kuwa ni pamoja na magonjwa mbalimbali yanayowakumba wanawake kabla na baada ya uzazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk. Geofrey Marandu alisema magonjwa hayo husababisha wanawake na watoto wachanga kukaa muda mrefu wodini hivyo  kusababisha msongamano mkubwa.

Alisema sababu nyingine ni ndoa za utotoni ambazo husababisha wanawake wenye umri mdogo kuzaa watoto wenye matatizo ya afya jambo ambalo linaongeza muda wa kukaa hospitali.

“Lishe na maandalizi duni ya uzazi kwa wanawake wajawazito inachangia kwa kiasi kikubwa upungufu wa damu na kupata shinikizo la damu linalosababisha kifafa cha mimba, hivyo mama kupewa rufaa kwenda hospitalini hapo.

Dk. Marandu alisema jitihada za ziada zinahitajika kupunguza msongamano huo ikiwa ni pamoja na kuimarisha hospitali za mikoa kwa kupeleka wataalamu wa kutosha katika hospitali hizo.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha MNH, Aminiel Eligaesha alisema hospitali hiyo ina vitanda 140 vya kulaza watoto wenye umri wa chini ya mwezi mmoja ambao hulazimika kulazwa na mama zao.

“Kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani huduma ya watoto chini ya mwezi mmoja inapatikana zaidi hapa, hivyo hupewa rufaa kuja hapa na kusababisha watoto wengi kulazwa zaidi ya vitanda tulivyonavyo.

“Mfano Aprili 17 mwaka huu, jengo la wazazi namba moja lilikuwa na wanawake 372 waliolazwa huku likiwa na vitanda 326 tu.

“Kati yao 228 walilala kwa sababu watoto wao walilazwa kwa matatizo mbalimbali hivyo wao walikuwa hapo kwa sababu ya kuwanyonyesha mara kwa mara,” alisema Eligaesha.

Alisema pamoja na msongamano huo picha zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya jamii zilipigwa siku ya usafi ambayo wagonjwa hutolewa nje kusafisha katika wodi hizo.

Wakati huo huo, Jumuiya ya waumini wa dhehebu la Shia nchini wamechangia fedha za upasuaji na matibabu ya watoto 40 waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa matibabu.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Azim Dewji alisema matibabu hayo yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki yatagharimu Sh  milioni sita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles