WAKATI tukikumbuka kifo cha mfalme wa muziki wa reggae, Robert Nesta ‘Bob Marley’, aliyefariki Mei 11, 1981 huko Miami, muziki wa reggae kwa Tanzania unaonekana kushuka kutokana na sababu mbalimbali.
Wanamuziki waliokuwa wakiimba muziki huo wengi wao wanaendeleza harakati nyingine tofauti na walivyokuwa wakifanya zamani kwa kuuendeleza muziki huo kwa kutoa nyimbo mbalimbali zenye mafunzo, hamasa na umoja.
Lakini wapo wengine wanauendeleza muziki huo kwa kuendelea na kutoa nyimbo mbalimbali lakini wanakosa nafasi ya kuchezwa kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini kutokana na sababu pia mbalimbali ikiwemo kutokuwa na vipindi vya kutosha vya kucheza muziki huo, pia kutokuwa na weledi wa waandaaji wa vipindi hivyo au kukosa hamasa kwa wasikilizaji wa vituo vya redio na runinga.
Kitu kikubwa kilichotakiwa na wanamuziki hao wa reggae ni kutokata tamaa kwa muziki wao kwa kuwa hata waanzilishi walianza muda mrefu bila mafanikio lakini baadaye walipata mafanikio makubwa kiasi kwamba kwa leo tunakumbuka kumbukumbu zao licha ya kufariki dunia.
Bob Marley alizaliwa Februari 6 mwaka 1945 huko Nine Mile, Saint Ann Parish nchini Jamaika.
Inaelezwa kwamba jina lake halisi ni Nesta Robert Marley, lakini kutokana na kukosewa kwa majina yake katika hati ya kusafiria akaendelea kutumia jina la Robert Nesta Marley.
Mama yake alikuwa mweusi, alifahamika kwa jina la Cedella Booker na baba alikuwa Mzungu aliyefahamika kwa jina la Norvall Marley, lakini baba yake alifariki mwaka 1955 kwa ugonjwa wa moyo akiwa na miaka 10 tu baada ya kifo hicho akawa akilelewa na mama yake.
Mama yake anaolewa tena
Licha ya kupenda muziki lakini alipokuwa na umri wa miaka 12, mama yake alimchukua Bob Marley wakahamia katika Jiji la Kingston ambako alianzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine, akapata watoto wawili, Bunny Wailer na binti yake Pearl.
Bob na Bunny wakaungana na kuendeleza muziki kwa kuiga muziki waliokuwa wakiusikiliza redioni, baadaye walikutana na Peter Tosh, Beverley Kelso na Junior Braithwaite na baadaye wakawa maarufu wakubwa duniani.
Februari 1962 nyimbo wa ‘Judge Not’, ‘One Cup of Coffee’, ‘Do You Still Love Me?’ na ‘Terror’ zilitungwa na kuingizwa sokoni na mwaka mmoja baadaye, Bob Marley, Bunny Wailer, Peter Tosh, Junior Braithwaite, Beverley Kelso na Cherry Smith wakaanzisha kundi la The Teenagers ambalo walilibadilisha na kuliita The Wailing Rudeboys kisha The Wailers.
Mwanzoni mwa mwaka 1964 waliuza nakala 70,000 wakati huo. The Wailers likawa kundi kubwa lakini mwaka 1966 baadhi ya wanamuziki walilikacha kundi hilo na kuwaacha wakongwe Bob Marley, Bunny Wailer na Peter Tosh.
Alijifunzaje muziki
Wakiwa shule ya msingi ya Stepney iliyopo Nine Mile, alikutana na rafiki yake Neville Livingston maarufu kwa jina la Bunny Wailer, kidogo kidogo walianza kujifunza muziki hadi walipoingia sekondari.
Ndoa na imani
Mwaka 1966, Bob Marley alimuoa Rita Anderson ambaye alijiunga katika kundi lake akiwa kama mwimbaji mwitikiaji.
Baadaye walihamia kwa muda nchini Marekani katika Jiji la Delaware huko akawa mfanyakazi katika kiwanda cha kutengenza magari cha Chrysler akawa akijiita Donald Marley huku akiendeleza imani ya kirastafari.
Aliporudi Jamaica akaingia rasmi katika Urastafarian na kuanza kufuga nywele kwa mtindo wa ‘dreadrocks’ imani hii ya kufuga nywele bila kukata inadaiwa inatokana na maelezo ya Biblia kuhusu Samson aliyeelezwa kwamba alikuwa na guvu za siri katika nywele zake za asili.
Mwaka 1976, Marley aliondoka Jamaica, akahamia Uingereza kati ya mwaka 1977 mpaka 1978 akiwa huko alirekodi albamu mbili ya Exodus na Kaya. Exodus ilikuwa kwenye chati za Uingereza kwa wiki 56 yaani mauzo yake yalikuwa kati ya albamu bora kwa wiki 56. Inasemekana aliuza nakala milioni 75 za albamu hiyo.
Siasa
Mwaka 1978 alirudi tena Jamaica kufanya concert jingine la amani lililoitwa ‘One Love Peace Concert’, mwisho wa onyesho kwa maombi ya Bob, viongozi wa kisiasa waliokuwa wakipingana na kupelekea wafuasi wao kuuana, Michael Manley (kiongozi wa chama kilichokuwa kikitawala wakati huo, People’s National Party) na Edward Seaga (kiongozi wa upinzani wa chama cha Jamaica Labour Party), wakashikana mikono.
Bob alirekodi kwa jina la Bob Marley and the Wailers albamu 11, albamu nne za live na saba za studio, ikiwemo Babylon by Bus, pia alisaidia maeneo mbalimbali yaliyokuwa na migogoro ya kisiasa kumaliza migongano yao.
Kifo chake
Julai 1977, Marley akakutwa na kitu kimeota chini ya ukucha wa mguu wake, kitu kilichoonekana na madaktari kuwa ni aina ya kansa, hivyo daktari wake akamshauri akatwe kidole lakini alikataa kwa madai kwamba dini yake hairuhusu.
Mei mwaka 1980, alikuwa ameshakamilisha ziara ya nje ya nchi lakini alipofika Milan, Italia alifanya  onyesho lililohudhuriwa na watu 100,000, alipomaliza akahamia Marekani akafanya maonyesho kadhaa lakini afya yake ilianza kuzorota kutokana na kansa kuenea mwili mzima.
Mei 11, 1981, alifariki katika Hospitali ya Cedars Lebanon alipokuwa na umri wa miaka 36 tu Mei 21 mwaka huo alizikwa na gitaa lake jirani na alipozaliwa kwa mazishi ya kitaifa na kadiri ya imani yake ya Urastafarian.
Imeandaliwa na Festo Polea kwa msaada wa mitandao ya kijamii.