28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm ageukia kazi ya kiume

hans-van-der-pluijm*Kujaribu silaha zitakazoiua Esperanca Jumamosi Taifa

NA EMMANUEL MALIMA, MBEYA

BAADA ya kujihakikishia ubingwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha mkuu wa timu ya Yanga Mholanzi, Hans Van De Pluijm, ameingia na gia mpya kwenye mechi ijayo Jumamosi dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo amepanga kukijaribu kikosi atakachokitumia nchini Angola dhidi ya Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Mei 17.

Mashabiki wa Yanga Jumamosi hii watashuhudia timu yao ikikabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.

Maamuzi hayo ya kocha huyo kujaribu kikosi hicho ni kama kuamua kugeukia kazi ya kiume ya michuano ya kimataifa, kwani kuchukua ubingwa wa ligi haikua kazi ngumu kwake.

Yanga inayopewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye makundi baada ya kushinda mabao 2-0 katika mechi ya kwanza hatua ya 16 bora michuano ya kombe hilo, imepania kujitengenezea mazingira ya ushindi kutokana na maandalizi inayoyafanya.

Pluijm aliliambia MTANZANIA mjini Mbeya kuwa katika mechi hiyo Yanga itawatumia wachezaji wake Wazimbabwe ambao hawakucheza mechi ya kwanza, akiwategemea kama silaha zake muhimu.

Yanga inasaka rekodi muhimu kwenye michuano ya kimataifa ili kuzima kelele za wapinzani wao Simba ambao wamekuwa wakijivunia kuingia hatua ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inawakejeli Yanga kwa mambo mawili; inawaambia Yanga kwamba wamebahatisha kuingia hatua hiyo na kwamba ndege yao ya mwisho Afrika ni pale watakapoifuata Esperanca kwao, lakini pia inawaambia hawawezi kufikia rekodi yao ya michuano ya Afrika kama wao, waliowahi kuitoa Zamalek ya Misri mwaka 2003. Lakini Pluijm amesema kutokana na maandalizi jinsi yalivyo, haoni kama kuna kikwazo kinaweza kuwazuia.

“Tumemaliza kazi ya ubingwa wa ndani sasa tunageukia kazi ya kimataifa. Na kwa jinsi tulivyojiandaa sioni kama wapinzani wetu wanaweza kutuzuia,” alisema Pluijm.

Mmoja wa vigogo wa Yanga amedokeza kwamba lengo lao ni kuingia kwenye hatua ya makundi na kurejesha hadhi ya Yanga ambayo imekuwa ikiipigania kwa misimu kadhaa ikiwa ni pamoja na kupigania ubingwa wa kihistoria kwa timu za Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles