Na Clara Matimo, Mwanza
Mwenyekiti wa Shughuli za Afya na Elimu katika Taasisi ya Aga Khan, Zahra Aga Khan amewasili jijini Mwanza leo Aprili 25,2023 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili lengo likiwa ni kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Afya inayofadhiliwa na kutekelezwa na Taasisi ya Aga Khan.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adama Malima baada ya kuwasili uwanja wa ndege, Zahra amesema anazifahamu vizuri nchi za Afrika Mashariki pamoja na vivutio viliyomo hivyo yuko tayari kushirikiana na uongozi wa mkoa huo kutangaza vivutio vya utalii vya mkoa huo ili uwe kitovu cha utalii kwa nchi za Afrika Mashariki na kati.
“Nilikuwa hapa Mwanza miaka 10 iliyopita nashukuru sana kwa mapokezi mazuri, niko kwenye ziara ya kikazi ya siku saba kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya Elimu na Afya inayotekelezwa na Taasisi ya Aga Khan katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
“Hivyo nakuhakikishia Mkuu wa Mkoa tutashirikiana kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya mkoa wako ili uwe kitovu cha utalii kwa nchi za Afrika Mashariki na kati,”amesema Zahra ambaye pia ni binti wa Aga Khan.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema hiyo itakuwa fursa nzuri kwa mkoa huo na taifa kwa ujumla katika kukuza uchumi wake kupitia sekta ya utalii nchini hasa ikizingatiwa kwamba uko karibu pia na vivutio vingine vya utalii ikiwemo Serengeti.
“Mradi wa ujenzi wa maendeleo ya kiwanja cha ndege ikiwemo jengo la abiria na mizigo ukikamilika uwanja huu wa ndege ukawa na hadhi kubwa ya kupokea abiria wa kimataifa tukasaidiwa na Zahra kutangaza vivutio vyetu hakika itasaidia sana kukuza sekta ya utalii nchini pamoja na uchumi wa wananchi wa mkoa wetu wa Mwanza,”amesema Malima.
Zahra atahitimisha ziara yake mkoani hapa Aprili 26 ambapo pamoja atatembelea pia jengo jipya la hospitali ya Aga Khan iliyojengwa eneo la Sahara jijini Mwanza.