26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 32 zilivyoinufaisha Ilemela mwaka mmoja wa Rais Samia

Na Clara Matimo, Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika Mkoa wa Mwanza, imepokea zaidi ya Sh bilioni 32 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni  na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla, kwenye maadhimisho ya siku 365 za Rais Samia, lengo likiwa ni kuelezea mafanikio yaliyopatikana wilayani humo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa kiongozi huyo.

Ameitaja miradi hiyo  ambayo imegusa sekta mbalimbali  na inayowanufaisha wananchi wa wilaya hiyo kuwa ni afya, maji, elimu, nishati, miundombinu ya barabara na upimaji wa ardhi.

Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, wilaya hiyo imepokea Sh bilioni 26 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi stendi kuu ya mabasi na malori iliyojengwa  eneo la Nyamhongolo na Sh milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari buzuruga.

“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, kwa kutoa fedha nyingi katika wilaya yetu ndani ya mwaka mmoja  ambazo zimegusa sekta mbalimbali, sasa hivi tuko bize tunatekeleza miradi kwa manufaa ya wananchi na hiyo ndiyo kiu kubwa ya rais wetu, tumepokea fedha Sh milioni 800 kujenga wodi hospitali ya wilaya, milioni 150 ujenzi wa zahanati tatu ambazo ziko kwenye kata zetu.

“Tulipokea Sh bilioni 1.94 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa hii imetuwezesha kujenga vyumba 97 vya madarasa ya shule za  sekondari kabla ya hapo hali ilikuwa ni ngumu baadhi ya wanafunzi walikuwa wanalazimika kusomea nje na kulikuwa na mrundikano mkubwa katika madarasa,”amesema na kuongeza

“Fedha hiyo ilitutaka tujenge vyumba vya madarsa pia tununue madawati lakini sisi tulienda mbali zaidi  fedha tuliyobakiza  tumejenga ofisi za walimu 28 ambazo hazikuwemo kwenye mpango kazi,  tumemalizia majengo ya shule ambayo wananchi waliyaanzisha, tumenunua madawati zaidi ya 1,000, tumeweka mpango kazi hadi Septemba mwaka huu hakuna mwanafunzi anayekaa chini wala anakosa sehemu ya kujifunzia,”alisema Masalla.

Amesema wanaendelea na zoezi la kupima viwanja na kumikikisha  wananchi maeneo mbalimbali  baada ya kupokea Sh bilioni 3.5 ambazo rais amewapatia  kama mkopo wenye masharti nafuu.

Masalla amesema kwa kasi ya maendeleo ambayo Rais Samia ameanza nayo, wananchi wa  Wilaya ya Ilemela watarajie mambo makubwa kutoka kwenye serikali ya awamu ya sita ikiwemo kumalizia kutekeleza miradi mikubwa ambayo tayari serikali imeisha toa fedha  ikiwemo ya maji na umeme.

“Ili tutekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati, wito wangu kwa wananchi wa Wilaya ya  Ilemela waendelee kutoa ushirikiano kwa mheshimiwa rais, viongozi wa mkoa, wilaya na kata  kwa kufanya hivyo watatupa mwanya wa kuwafikishia yale ambayo wanayatamani na ambayo Rais Samia anayataka kwa wananchi wake maana lengo la rais wetu ni kuwatatulia wananchi wake changamoto mbalimbali zinazowakabili,”amesema Masalla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles