24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa yatoa mikopo ya milioni 127

Na Samwel Mwanga, Maswa

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeendelea kutekeleza lengo la kuboresha hali ya maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa vikundi 24 yenye thamani ya Sh milioni 127  kwa Vijana, Wanawake na Walemavu kwa kipindi cha mwaka 2021/2022.

Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani wa Simiyu, Aswege Kaminyoge (kushoto) akimkabidhi ufunguo wa pikipiki ya magurudumu matatu,Mwenyekiti wa kikundi cha Vijana Cha Uzunguni mjini Maswa,Dietrich Mutechura(kulia)ukiwa ni mkopo toka halmashauri ya wilaya ya Maswa (Picha Na Samwel Mwanga).

Mikopo hiyo ni kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya ndani yanatengwa kwa ajili ya kuyawezesha makundi hayo ili waweze kutekeleza shughuli zao za ujasiliamali wenye tija.

Hayo yameelezwa Aprili Mosi, 2022 na Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo,Mercy Ndutu wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki mbili za magurudumu matatu kwa vikundi viwili vya Vijana kwa ajili ya kukusanya takataka katika mji wa Maswa.

Akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo kwa vikundi hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii, Mercy Mercy amesema kuwa vikundi 12 vya wanawake vyenye jumla ya wanachama 190 walipatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 52.8.

Amesema vikundi 7 vyenye wanachama 68 vilipatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 52.8 na Vikundi 5 vya watu wenye ulemavu vyenye wanachama 29 vilipatiwa mikopo yenye thamani ya Sh 21.4.

“Manufaa yanayotarajiwa baada ya kutoa mikopo hii ni pamoja na kuwezesha vikundi kupanua mitaji, kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitakazo kidhi mahitaji ya soko na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa walengwa,” amesema Mercy.

Amesema kuwa vikundi hivyo ambavyo vimekabidhiwa pikipiki hizo kwa ajili ya kufanya usafi katika mji huo ni miongoni mwa vikundi saba ambavyo vilipata mkopo katika kipindi  hicho yenye thamani ya Sh milioni 16 ambapo kila kikundi kilipatiwa mkopo wa Sh milioni 8.

“Vikundi hivi viwili ambavyo ni Kikundi cha Umoja wa Vijana Uzunguni na Kikundi cha Ushirikiano cha Vijana Shanwa kila kikundi kilipatiwa mkopo wa Sh Milioni nane na wamenunua pikipiki hizi kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Usafi wa Mazingira katika mji wa Maswa katika Kata za Binza, Sola, Shanwa na Nyalikungu,” amesema.

Amesema manufaa mengine yatakayotokana na mikopo waliyotoa kwa vikundi hivyo ni pamoja na kuchochea utengenezaji na upatikanaji wa ajira kwa vijana, kuwaepusha wanufaika na vitendo hatarishi vinavyochochea mmomonyoko wa maadili na uvunjifu wa amani, ukuaji wa uchumi wa kaya na jamii na kupunguza umasikini.  

Aidha, kupitia mikopo hiyo halmashauri hiuo itaongeza mapato kupitia vyanzo vyake vinavyoelekeana na shughuli za wajasiliamali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye pia ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki hizo amevitaka vikundi vilivyopokea mikopo hiyo ambavo ni vya vijana kuitumia mikopo hiyo kwa lengo lililokusudiwa na kuonyesha mfano wa kuigwa kwa vijana wengine na kuhakikisha mji huo unakuwa ni miongoni mwa miji misafi hapa nchini.

Amesema ili kufanya zoezi la utoaji mikopo kwa vikundi liwe endelevu kwa halmashauri ni vizuri vikundi vyote vilivyopatiwa mikopo mbalimbali kurejesha kwa wakati ili na vikundi vingine viweze kukopeshwa.

“Halmashauri ili zoezi la utoaji mikopo iwe endelevu fuatilieni vikundi vyote mlivyovipatia mikopo ili warejeshe kwa wakati na wengine waweze kukopeshwa utoaji wa elimu kwenye vikundi husika ili watumie fedha kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Hii itaondoa tatizo la vikundi kufanya matumizi ya fedha za mikopo yasiyoendana na malengo ya mikopo sambamba na hilo uhamasishaji uendelee  kufanyika ili vijana wajiunge kwenye vikundi na kuanzisha miradi yenye tija kusudi wapate sifa ya kuomba mikopo inayotolewa na Halmashauri,” amesema Kaminyonge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles