Na PENDO FUNDSHA
-MBEYA
BENKI ya TPB imejipanga kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo kama njia ya kupanua wigo wa biashara na ukuzaji uchumi wa Tanzania ya viwanda.
Kutokana na hali hiyo, benki hiyo imewataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali wanazozitoa, ikiwamo mikopo ya gharama nafuu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa wa Benki ya TPB Tawi la Mwanjelwa, jijini Mbeya, Mustafa Mmanga, kwenye kilele cha Maonyesho ya Wakulima za Nyanda za Juu Kusini (Nanenane), zilizofanyika katika uwanja wa John Mwakangale, alisema benki hiyo imejipanga vema katika ukuzaji wa pato la Mtanzania kupitia huduma mbalimbali wanazotoa.
“Riba ya mkopo huu ni asilimia tatu na unatolewa katika vikundi vya watu watano watano kwa kiasi cha fedha kinachoanzia shilingi 350,000 hadi 500,000 na milioni 1.5 kwa mtu aliye kwenye kikundi,” alisema Mmanga.
Alisema kazi kubwa inayotakiwa kufanywa na wanavikundi ni kuhakikisha wanaaminiana na kwamba ni watu wanaojishughulisha na biashara ndogondogo, kwani mkopo huo unatolewa kwa malengo husika na utatakiwa kurejeshwa ndani ya mwezi mmoja.
“Taasisi hizi za fedha, hasa benki hii ya serikali ilichelewa kuleta fursa hii na kuyaacha mashirika binafsi yakitekeleza mpango wa utoaji mikopo kupitia vikundi kwa riba kubwa ya asilimia 25, hali inayomfanya mwananchi kushindwa kunyanyuka kimasha,” alisema.
Alisema riba ya asilimia 25 ni kubwa sana, hivyo kama TPB benki itajipanga vizuri katika suala zima la utoaji elimu kwa wajasiriamali, basi itaweza kutekeleza sera ya kukuza uchumi kupitia viwanda vidogo kwa asilimia 100.
“Wajasiriamali wengi wanakosa mitaji na ndiyo maana bado wanaendelea na biashara zisizo na tija wala zisizokidhi viwango vya ubora, hivyo kushindwa kuhimili soko la ushindani la ndani na nje ya nchi,” alisema.