Na Walter   Mguluchuma-Katavi
WAMILIKI  na madreva wa  bajaji wanaofanya  shughuli za usafiri katika Manispaa ya  Mpanda mkoani Katavi,wamefanya  mgomo na kusitisha kutoa huduma za usafiri  katika maeneo ya  Manispaa ya Mpanda na  nje ya   Manispaa baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi na Majini ( SUMATRA), kupiga marufuku bajaji kufanya  safari zake kupitia  barabara kuu.
Mwenyekiti wa  wa   madreva wa   Bajaji, Rashid  Juma  alisema wameamua kusitisha kutoa huduma ya usafiri kwenye maeneo ya Manispaa ya  Mpanda, baada ya SUMATRA kupiga marufuku  bajaji zote ili kupunguza wingi wa ajali.
Alisema wameamua kusitisha huduma hiyo kuanzia juzi, ingawa walikuwa wamepata agizo, bali  wamesitisha kutoa huduma kwenye   maeneo yote  hata yale ya barabara ndogo.
Alisema kitendo cha kuwazuia, kitawafanya wakose mapato na kusabisha  kushindwa kulipa kodi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenyekiti wa wasafirishaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa   Kamati ya Usalama Barabarani wa Mkoa wa  Katavi, Nassor  Arfi alisema amepata taarifa za  kusimamishwa huduma  za usafiri wa   bajaji kupita kwenye  barabara kuu za  Mpanda- Kigoma,Mpanda Sumbawanga  na  Mpanda – Tabora na  amefanya mawasiliano na  Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Raphael Muhuga.
Alisema mkoa huo, hauna nyingine   mbadala  za kuwafanya  madreva wa majaji  kutumia, hivyo ni  vema  mamlaka hiyo ikatumia  busara kumaliza suala hilo.
Meneja wa SUMATRA wa  Mkoa wa  Katavi, Amani Mwakalebela alisema mambo yote yanaendeshwa kwa sheria halali.
Mkazi wa Mtaa wa Kazima, Aglipina Petro alisema   ameshindwa kumpeleka  mgonjwa wake hospitali, baada ya kukosa huduma ya usafiri.
Mkazi wa Kijiji cha Ibindi, Joice Longino  alisema kitendo cha   bajaji kusitisha huduma ya usafiri kumesababisha  wafanyabiashara  kushindwa  kufika mjini  Mpanda kununua bidhaa kwa  ajiri ya biashara zao.