24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HAMAD RASHID AIFUNDA BENKI YA KILIMO

Na MWANDISHI WETU

-LINDI

WAZIRI wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, ameiasa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwezesha wakulima ili waweze kuchangamkia fursa za kuuza mazao ya kilimo nje ya nchi, ili kuwaongezea kipato wakulima hao.

Waziri Hamad aliyasema hayo jana, alipolitembelea Banda la TADB, katika Viwanja vya Ngongo, mjini Lindi, wakati wa Maonyesho ya Nanenane yanayoendelea mjini humo.

Alisema kuwa, Tanzania inapata fursa nyingi za masoko nje ya nchi kwa mazao mbalimbali, ikiwamo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde, ikiwamo dengu na mbaazi, zinazotakiwa sana nchini India na Arabuni.

“Naiomba Benki ya Kilimo kuwawezesha wakulima wanaolima kibiashara ili kuchangamkia fursa za masoko kwa mazao ya kimkakati, yakiwamo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde, ikiwamo dengu na mbaazi ambazo nchi nyingi marafiki wanahitaji,” alisema Hamad.

Alisema wizara yake inaletewa maombi mengi ya mazao kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nchi hizo.

“Naamini benki hii ikiwawezesha wakulima wanaweza kuchangamkia fursa za masoko ya nje, ikiwemo ya wafanyabiashara kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu wanaohitaji zaidi ya kontena mbili za korosho kwa wiki,” alisema.

Akizungumza wakati wa akipokea ugeni huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga, alisema lengo la kuanzishwa kwa TADB ni kuchagiza juhudi za serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.

Alisema katika kutekeleza hayo, Benki ya kilimo imedhamiria na kujizatiti katika kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha, ikiwa ni pamoja na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunachagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.

Assenga alisema benki yao imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa sekta hizo, ili kuongeza tija kupambana na umaskini nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles