28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TIZEBA AZUNGUMZIA KODI ZILIZOFUTWA KWA WAKULIMA

Na MWANDISHI WETU

-LINDI

SERIKALI imesema imefuta baadhi ya kodi na tozo ili kuwanufaisha wakulima wote nchini ambao awali walikuwa wakilalamikia na kupinga tozo na kodi hizo kwa madai kuwa zilikuwa zikiwanyonya na si kuwakwamua na wimbi kubwa la umaskini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, wakati wa Maonyesho ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.

Alisema kuwa, kwa muda mrefu serikali imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali, hususan kwa wakulima nchini Tanzania, wakipinga kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa, kwani zimekuwa zikiwanyonya badala ya kuwakwamua na wimbi kubwa la umaskini, jambo ambalo serikali ililitazama na kuona umuhimu wake na hatimaye kufikia utekelezaji huo.

Dk. Tizeba alisema jumla ya tozo 80 kati ya tozo 139 zimefutwa na tozo nne  zimepunguzwa viwango.

Alisema tozo, kodi na ada zinajumuisha  kufutwa kwa tozo 12 kupunguza viwango kwenye zao la tumbaku. Kwenye zao la kahawa zimefutwa tozo 17 na moja kupunguzwa kiwango; sukari zimefutwa 16; pamba tozo zilizofutwa ni mbili,  kwenye korosho tozo mbili zimefutwa na chai imefutwa tozo moja.

Katika kuongeza upatikanaji wa pembejeo, tozo tatu zimefutwa na moja imepunguzwa kiwango kwenye mbolea na  tozo saba zilizokuwa kwenye mbegu nazo zimefutwa. Katika ushirika jumla ya tozo 20 zimefutwa katika ngazi mbalimbali.

“Katika mifugo kodi, ada na tozo saba ambazo zilikuwa kero kwa wafugaji, wafanyabiashara na wawekezaji nazo zilifutwa na kubakiza zile tu zenye uhusiano wa moja kwa moja katika uendelezaji wa Sekta ya Mifugo. Tozo zilizofutwa zinajumuisha mbili kwenye maziwa; nyama tozo nne na moja kwenye afya ya mifugo,” alisema Dk. Tizeba.

Alisema katika Sekta ya Uvuvi, jumla ya kodi, ada na tozo tano ambazo ni kero kwa wavuvi, wafugaji wa viumbe kwenye maji na wawekezaji nazo zimefutwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema kwa sasa Serikali itaendelea kuchambua kwa kina tozo, ushuru na ada mbalimbali zilizobaki katika kilimo, mifugo na uvuvi, kwa lengo la kuangalia uhalali wa kuwapo kwake ili kuwapunguzia wakulima, wafugaji na wavuvi mzigo wa tozo, ushuru na ada zisizokuwa na tija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles