Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
WAKATI Serikali ya Tanzania ilipotoa tamko la kuyataka makampuni na mabenki mbalimbali nchini ambayo yalikuwa bado hayajasajiliwa rasmi yajisali ifikapo mwaka 2017, hatimaye Benki ya Posta (TPB Plc) imeshakamilisha zoezi hilo.
Kutokana na usajili huo, benki hiyo imeweza kubadili nembo yake ya awali na sasa imebadilika na kutumika kuanzia Januari 19, mwaka huu na jina lake kuwa TPB Plc.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPB Plc, Sabasaba Moshingi, anasema mabadiliko hayo yanakwenda sambamba na mabadiliko makubwa yanayotokea ndani ya benki hiyo.
Anaendelea kusema kuwa mabadiliko ya kibenki yalianza kutekelezwa toka mwaka 2001 kwa kuanza na kuchagua upya viongozi lakini kwa bahati nzuri, ninashukuru Mungu nilichaguliwa na mpaka leo nipo katika kitengo hiki.
“Vilevile tulibadilisha mwonekano wa matawi zaidi ya 28 hapa nchini na kuwa ya kisasa katika mikoa mbalimbali, tulibadilisha mfumo wa utoaji wa huduma kwani kwa kipindi hicho tulikuwa katika benki nyingi, vilikuwa vikitumika vitabu lakini ni tofauti na sasa kwani kuna teknolojia mahususi ambayo hutumika zaidi katika mabenki mengi,” anasema
Pia anasema TPB wameimarisha huduma ya kibenki kwa njia ya simu kutoka kwenye benki na kwenda katika simu ya kiganjani (simbankig).
Anasema kuna huduma nyingine nyingi ambazo wameziunganisha kwa ajili ya kinamama, mojawapo ni njia ya vicoba, kwa maana hiyo badala ya kuweka fedha katika vibubu wana uwezo wa kuhifadhi benki.
“Benki hiyo imeweka mfuko wa wastaafu wa wafanyakazi iliyokuwa Posta kiasi cha Shilingi bilioni 77, pia imejenga nyumba katika Mkoa wa Njombe kwa ajili ya watu wasiojiweza,” anasema Moshingi.
Anasema benki yake imekamilisha mchakato wake wa muda mrefu wa kuisajili benki hiyo chini ya sheria ya kampuni, ambapo mchakato huo ulikamilika toka mwaka jana na hivi sasa benki hiyo inaitwa TPB Bank plc.
“Benki iliamua kuanzisha kubadilisha nembo yake ili kwenda sambamba na jina hilo pamoja na mabadiliko makubwa ya kuiboresha benki hii yanayoendelea,” anasema Moshingi.
Aliishukuru sana Wizara ya fedha kwa ushirikiano huu kuzidi kuendelea baina yao hususani katika kipindi hiki ambapo benki ipo katika mchakato wa kuingia katika soko la hisa.
Anasema lengo na madhumuni hasa ni kupata mtaji ili benki iweze kujiendesha yenyewe kwa ufanisi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TPB Plc, Prof. Lettice Rutashobya, alimhakikishia Waziri wa Fedha kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake ili kufikia maendeleo zaidi.
Prof. Rutashobya anasema vilevile ataweka jitihada zaidi ili kuwafikia Watanzania wengi hususani wale walioko pembezoni ili nao waweze kufaidika na huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
“ Ingawa tuna changamoto ya mtaji wa kutosha wa kuwafikia wananchi, asilimia 14 pekee ndiyo huduma iliyowafikia wananchi katika benki yetu lakini,” anasema Prof. Lutashobya.
Anasema tumeanza mchakato wa kuungana na benki nyingine nchini kwa lengo la kuikuza na kuiendeleza benki yetu ili iweze kuwa juu zaidi kimaendeleo.
Uzinduzi huo ambao ulifanywa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dr. Phillip Mpango na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi mbalimbali nchini na Waziri aliupongeza uongozi wa benki kwa hatua waliyofikia ya kuweza kuthubutu katika kuikuza na kuiendeleza benki hiyo.
Anasema: “Nimeona baadhi ya benki nyingi nchini zimeendelea kukua kimaendeleo kwa utoaji wa huduma za kibenki kwa wananchi.
“Kitu ambacho kimenivutia zaidi katika benki zote ni kuongezwa kwa mashine za kutolea fedha, yaani (ATM) na huduma za simu.
“ Serikali inamini kuwa katika maendeleo ya miaka hii katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vya kati, ili tuwe na Tanzania ya viwanda,” alisema Mpango.
Vile vile Mpango anasema matarajio ya Serikali kwa makampuni na benki zote nchini ni kupitia huduma hiyo kuwafikia wananchi hadi vijijini.
“Kama tatizo ni mtaji inabidi mjitahidi zaidi kwa hali na mali kutafuta vyanzo mbadala ambavyo vitawezesha upatikanaji wa mtaji huo ili kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi,” anasema Mipango.
Anasema wakifanya hivyo watakuwa wazalendo wakubwa nchini kwa kuanza na nyumbani kwanza, kwa kununua vya kwao.
Hata hivyo, aliwaomba Watanzania wote kuwa na huduma hii itakapofika sokoni kuuza hisa kwamba Watanzania wawe wa kwanza kununua hisa hizo.
“Katika suala la mtaji nina imani tutaendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana kwa pamoja ili tuweze kufanikisha na wananchi waweze kufaidika,” anasema Mpango.
Vile vile ameiasa bodi ya benki hiyo kutengeneza utaratibu wa kutoa mikopo kwa wananchi ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma.
Anasema” Sisi kama Serikali tutaendelea kutoa ushirikiano kwenu ili hatimaye benki hii ijiimarishe kimtaji na kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa benki hii imefanikiwa kwa kupeleka huduma zake za kibenki hadi pembezoni mwa nchi, kwa kujenga matawi yenu kwenye miji mikuu karibu yote nchini pamoja na kufikisha huduma yenu ya TPB popote,” anasema Dk. Mpango.