23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya Mwalimu kukopesha wafanyakazi vifaa vya ujenzi

*Lengo nikuwasaidia waweze kumiliki nyumba zao

Na Christina Galuhanga, Mtanzania Digital

KATIKA kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya watumishi, Benki ya Mwalimu Commercial PLC, imejidhatiti kuwakopesha wafanyakazi vifaa vya ujenzi ili waweze kufikia malengo ya kumiliki nyumba na kuboresha makazi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bidhaa yao mpya ya Jenga na Mwalimu Benki kwa kushirikiana na kampuni ya Wasambazaji na Wauzaji wa Vifaa vya ujenzi ya Wahenga (FMJ),Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko wa Benki hiyo, Sabina Mwakasungura amesema, mkakati huo utasaidia watumishi wa umma na binafsi kunufaika kwakuwa huduma hizo zitatolewa kwa bei nafuu na zenye tija.

Amesema Benki hiyo katika kuendana na mpango mkakati wa miaka mitano imelenga kuboresha huduma zenye ubunifu na ufanisi katika kuwafikia wateja huku moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kuwa na bidhaa zinazolenga moja kwa moja watumishi wa kada zote ili wajiinue kiuchumi na kuleta tija ndani ya jamii.

“Benki yetu imelenga katika utoaji wa huduma za kibenki ambazo ni nafuu salama na zinazopatikana popote na wakati wowote kwa njia ya kidigitali pamoja na Mwalimu Mobile, Mwalimu wakala na Mwalimu Card Visa,” amesema Sabina.

Ameongeza kuwa huduma hizo zinawezesha wateja waliosambaa mikoa yote kufanya miamala kwa urahisi bila usumbufu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Abdallah Kirungi amesema, hadi sasa Benki hiyo ina matawi mawili Dar es Salaam na mengine tisa Katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha, Rukwa, Kigoma, Mtwara na Arusha.

Amesema matarajio ya benki hiyo ni kuwa na vituo katika mikoa yote ifikapo mwaka 2025.

Amesema kama Benki wametoa fursa hiyo kwa wakopaji kukopa kiasi chochote ili mradi mteja awe na uwezo wa kulipa mkopo huo.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Wasambazaji na wauzaji wa vifaa vya Ujenzi ya Wahenga ( JMF), Fatna Senzota ameipongeza Benki hiyo kwa wazo hilo na kuwashauri kuangalia kwa upana zaidi kutoa fursa hizo kwa sekta nyingine.

Amesema zipo shule binafsi na sekta nyinginezo ambazo watumishi wake wanahitaji mikopo ya bei nafuu ili waweze kuboresha maisha hivyo kufanya hivyo kutasaidia kuinua uchumi wa nchi na maisha ya jamii kwa ujumla.

” Ni wakati sasa kwa watumishi kutumia fursa hii ya hitaji lao kubwa la ujenzi kwa njia ya mkopo ambapo masharti yake ni nafuu na vifaa vyake ni bora,” amesema Sabina.

Amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma hiyo ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu sasa na wana matumaini mkakati huu mpya utawafikia wengi na utasaidia wengi kuondokana na changamoto ya ukosefu wa makazi.

Pia, Mshauri wa Kampuni hiyo, Wema Muhama amesema, ni wakati sasa kwa watumishi kunufaika na bidhaa hizo ambazo tayari zipo sokoni na zinapatikana kwa bei nafuu.

Amesema tamaa yao kubwa ni kuona maisha ya watumishi na watanzania kwa ujumla yanabadilika kupitia mpango huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles