27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wataka kuundwa chombo huru cha kusimamia Tasnia ya Habari

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

WADAU wa Tasnia ya Habari nchini wameendelea kutoa maoni yao juu ya vifungu ambavyo imekuwa vikikwamisha sekta hiyo kutokuwa na viwango vya kimataifa.

Maoni hayo yanakuja kufuatia kuwapo kwa Shria ya Huduma za Habari nchini ambayo imekuwa na baadhi ya vifungu vinavyominya vyombo vya habari nchini.

Mwenyekiti wa Jukuwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile.

Akizungumza na Mtanzania Digital Juni 7, 2022 mmoja wa wadau hao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania(TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa kuna mambo mengi yanayopaswa kubadilishwa ili kuifanya tasnia hiyo kuwa huru.

“Tukiangalia vifungu viwili ambavyo ni namna 9 na 10, tunaona kwamba kifungu cha 9 kinampatia mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) kusajili na kufuta leseni za magazeti jambo ambalo katika sheria ya magazeti namba 3 ya mwaka 1976 iliyofutwa mwaka 2016 kitu hiki kilikuwa chini ya kifungu cha 25 ambapo mamlaka haya yalikuwa mikononi mwa waziri.

“Lakini tulivyopiga kelele sana, jamii ikasema hapana, jambo hili siyo jema, nadhani serikali ikasikia kelele za wananchi ikaondoa mamlaka haya kwa waziri, lakini kwa mashangao mamlaka haya kupitia mlango wa nyuma yakapelekwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo).

“Sasa unaweza kujiuliza kwamba hakuna utaratibu uliowekwa wala hamna chombo kinachomdhibiti katika kufuta wala kutoa leseni sasa tukasema haiwezekani yeye huyo akawa mlalamikaji, akawa mwendesha mashtaka na akawa mto huku katika kesi inayomhusu ndiyo sababu tukasema kwamba kuwapo na chombo maalum kitakachokuwa kinasimamia maadili na kazi ya uandishi wa habari nchini,” amesema Balile.

Balile amefafanua kuwa kuundwa kwa chombo hicho kitasaidi mtu yeyote mwenye malalamiko ikiwamo serikali au Taasisi kama ilivyo nchini Kenya.

“Sasa ukiangalia hapa kwetu mamlaka haya yapo mikononi mwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo) na tumeshuhudia jinsi mamlajka haya yalivyotumiwa vibaya dhidi ya magazeti ya MwanaHalisi, Mawio , Mseto na Tanzania Daima, kwa hiyo hili tunalolizungumza ni hatari ya kweli ambayo ipo, hivyo tunasema hili hapana.

“Ukienda kifungu cha 10 kinasema kwamba iwapo mmiliki wa chombo cha habari atakuwa hakubaliani na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo) basi akate rufaa kwa waziri mwenye dhamana jambo ambalo ni mchezo uleule.

“Kwani kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107 chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki kwa mujibu wa sheria ni mahakama, hivyo kitendo cha waziri, Mkurugenzi kupewa mamlaka ya kikatiba nje ya mfumo wa mahakama hiyo nayo tunaona haijakaa sawa tunadhani kama wenzetu walivyo na chombo huru basi nasi tunapaswa kufanya hivyo.

“Lakini itoshe tu kusema kwamba hatukubaliani na utaratibu wa mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo) kutoa leseni, kufuta leseni, kustisha leseni bila mtu kulalamika kwa mtu yeyote pale anapojisikia kufanya hivyo kwani sheria ya sasa inampa mamlaka hayo,” amesema Balile.

Katika hilo Wakili James Marenga amebainisha kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi.

“Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi na ni jambo lisilohitaji msisitizo mkubwa sana kwa sababu umuhimu wake unajulikana.

“Hivyo, kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya serikali na umma,”amesema Marenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles