BEATRICE KAIZA
KAMPUNI ya Multichoice Tanzania kupitia huduma zake za DStv imechukua sura mpya baada ya Benki maarufu nchini KCB kutangaza kudhamini mashindano ya michuano ya Ndondo Cup 2020 ambayo tayari imeshaanza na itaendelea hadi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa kitengo cha masoko Multichoice Tanzania, Baraka Shelukindo amesema kuwa uzito na umuhimu wa mashindano ya Ndondo Cup kwa jamii ni mkubwa ndio maana wameamua kuingia kwenye mashindano na yataonyeshwa kupitia Plus tv chaneli namba 294 kwenye king’amuzi cha DStv.
“Mwaka huu kutokana na uzito wake ambayo mashindano haya yamekuwa nayo kwa jamiii, sisi DStv Tanzania, KCB Bank, na Plus Tvtz tukaona ni jambo kubwa ambalo hatuwezi tukaliacha lipite hivi hivi, tuweke mkono wetu tuingie na kushirikiana na waratibu na ndondo ambayo inatoka kuonekana Tanzania pekee na inakwenda Kimataifa, waafrika wanaotumia kinga’amuzi cha DStv hata nje ya nchi wataweza kuona Ndondo Cup, pia ni faida kwa wachezaji sababu wataonekana zaidi ya nchi 30 Afrika nzima, ” amesema Shelukindo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario, amesema kuwa benki yao imeamua kudhamini NdondoCup kwasababu imekuwa ni chimbuko la vipaji vya wanasoka vijana hapa nchini.
“Kutokana na mafaniko ya mashindano hayo katika kukuza na kuibua vipaji ndiyo sababu tumeamia kudhamini Ndondo Cup ili iweze kuwa ya kiwango cha juu zaidi na hatimaye kuweza kuzalisha wachezaji wazuri na mahiri ambao wanaweza kuchezea timu kubwa za ndani na hata timu za taifa,” amesema Cosmas Kimario.