33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya Dunia yaanika hali ya umaskini nchini

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MATOKEO ya tathmini ya kina ya umaskini kwa kutumia yale ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara ya mwaka 2017/18 na vyanzo vingine kutoka katika tafiti zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki ya Dunia yanaonyesha ndani ya miaka minne umaskini umepungua kwa asilimia mbili.

Hayo yalibainishwa jana Jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa wakati akizindua matokeo ya utafiti huo.

Matokeo yameonyesha kuwa umaskini wa mahitaji muhimu  umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007,  asilimia 28.2 mwaka  2012, hadi asilimia 26.4 mwaka 2018.

Umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 22 mwaka 1991/92, asilimia 19 mwaka 2000/01, asilimia 17 mwaka 2007, asilimia 10 mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

Awali katika taarifa yao kwenye vyombo vya habari, Benki ya Dunia ilimkariri Bella Bird, ambaye ni Mkurugenzi mkaazi akizungumzia ripoti hiyo akisema; “kupungua zaidi kwa umaskini ni habari njema,” lakini alitoa tahadhari ya kundi kubwa la Watanzania kurudi kwenye umaskini.

Alisema ni muhimu kwa Tanzania kupambana na hali ya umaskini, kwani idadi ya maskini bado iko juu na idadi kubwa ya watanzania wako katika hatari ya kurudi kwenye umasikini kwa kiwango kidogo.

Aidha katika taarifa hiyo Benki ya Dunia ilieleza kuwa karibu nusu ya idadi ya watu nchini Tanzania kila mmoja  anaishi chini ya dola 1.90 kwa siku

“Kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kufanya huko mbele ya kuboresha hali ya maisha kwa watu wote.”

Tathmini pia inaonyesha ishara ya kuibuka mabadiliko ya kimuundo ambayo yanaweza kuonekana katika eneo la viwanda na huduma katika ajira kwa ujumla.

Kuhusu sekta ya kilimo  ripoti hiyo imeonyesha kuwa kinaajiri watu wachache na wale ambao hubaki kwenye sekta hiyo wanajitanua kuelekea kujiajiri na kutojilipa mshahara.

Miongoni mwa matokeo mengine muhimu, tathmini inaonyesha kuongezeka kwa umiliki wa mawasiliano na mali ya uchukuzi na pia katika upatikanaji wa huduma za msingi kama huduma ya maji iliyoboreshwa, huduma za usafi, nishati na mtandao wa barabara

Pia kiwango cha udahili mashuleni kimeelzwa kimeongezeka, na sehemu kubwa ya nguvu ya wafanyakazi inafanya kazi katika sekta za juu zaidi na juu.

Pamoja na maboresho haya, ripoti hiyo imeonyesha kiwango cha jumla cha elimu na upatikanaji wa huduma za msingi kimebaki chini, hasa kwa maskini na kwa wale wanaoishi vijijini.

Kwamba hii inatoa taswira katika katika ukuaji wa hivi karibuni kuwa duni-maskini na kupanua pengo la ustawi kati ya matajiri na maskini.

Pamoja na hayo, ripojti pia imeonyesha kuna ishara ya kuongezeka kwa ushiriki wa maskini  kwenye uzalishaji, licha ya kwamba  wanaendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa ujuzi na uwezo na upungufu wa fursa bora za kazi.

Ongezeko kubwa la idadi ya watu  nalo limetajwa kama changamoto kubwa katika juhudi za kupunguza umasikini Tanzania.

Pamoja na ongezeko hilo, Benki ya Dunia imesema inaweza kuwa nafasi kubwa  ya nchi kufanya uwekezaji sahihi na mipango ya sera.

WAZIRI BASHUNGWA

Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri Bashungwa alisema Novemba 20,2015 siku ambayo Rais John Magufuli alifungua Bunge, kati ya vipaumbele alivyosema Serikali yake itavishughulikia kwa nguvu zote ni pamoja na kupunguza umaskini.

Alisema Rais Magufuli alipoingia madarakani umaskini wa mahitaji ya msingi ulikuwa asilimia 28.2. Katika kipindi cha takribani miaka minne umepungua na kufikia asilimia 26.4.

Alisema kupungua huko ni matokeo ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma za jamii ambazo ni pamoja na maji, elimu, afya, barabara na nyinginezo.

“Sote ni mashahidi kasi ya Mfumuko wa Bei wa Taifa wa bidhaa na chakula umeendelea kuwa wa tarakimu moja ambapo mwezi Oktoba, 2019 ulikuwa asilimia 3.6.

“Hali ya kuwa na chakula cha kutosha nchini ni faraja kubwa sana kwa Serikali na Wananchi wake”.

“Hizi ni juhudi kubwa zilizofanyika kwa kipindi kifupi…kama tunavyofahamu, umaskini ni suala mtambuka, hivyo kupambana nalo kunahitaji jitihada zilizoratibiwa vyema katika sekta zote za uchumi, ” alisema.

Alisema matokeo yameonesha asilimia 73 ya kaya za Tanzania Bara kwa mwaka 2017-18 zilitumia maji ya kunywa kutoka vyanzo bora vya maji katika kipindi cha kiangazi ukilinganisha na asilimia 61 mwaka 2011/12.

Hata hivyo, utafiti unaonesha tofauti ipo katika matumizi ya maji kwenye maeneo ya vijijini ambapo asilimia 65 ya kaya zilitumia maji ya kunywa kutoka vyanzo bora vya maji katika kipindi cha kiangazi mwaka 2017-18 ukilinganisha na asilimia 52.5 mwaka 2011/12 na maeneo ya mjini ni asilimia 87.6 mwaka 2017-18 ukilinganisha na asilimia 78 mwaka 2011/12.

Waziri Bashungwa alisema hiyo ni hatua kubwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kaya zote nchini kupata maji ya kunywa kutoka katika vyanzo bora.

Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Wananchi wote wanapata maji ya kunywa yaliyo safi na salama kwa asilimia 100.

Kuhusu kipato, alisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuboresha kipato na hali ya maisha ya watu hasa katika makundi maalum kama wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa kuziagiza halmashauri zote kutenga asilimia kumi ya mapato yao kwa ajili kukopesha vikundi vya uzalishaji mali kwa makundi hayo bila riba.

Akizngumzia umuhimu wa matokeo hayo alisema watunga sera, waratibu wa miradi na wadau wengine yanawasaidia kufuatilia na kufanya tathmini ya mipango na miradi iliyopo.

“Yatasaidia pia kutathmini na kufuatilia hatua tulizofikia katika utekelezaji wa malengo mbalimbali ya nchi, kikanda na yale ya kimataifa, yana taarifa nyingi zinazohusiana na ustawi wa kaya katika nchi yetu,”.

Alisema matokeo ya utafiti yametoa matumaini na kuonesha matokeo chanya ya juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano na wadau wengine katika kupunguza kasi ya kiwango cha umaskini nchini.

Alitoa rai kwa wananchi wote kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia shughuli zao mbalimbali za uchumi kwa lengo la kustawisha kaya zao na kuboresha maisha yao ya kila siku na kwamba jukumu la Serikali ni kujihakikishia wanatoa fursa sawa kwa wananchi wote.

Bashungwa pia alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo lengo lake kuu ni kuondoa umaskini na kukuza uchumi na kuwasihi viongozi kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi.

“Tukumbuke mwaka 1991/92 kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kilikuwa asilimia 39.0. Ndani ya miaka 26 kiwango cha umaskini kimeweza kupungua kwa asilimia 13,”alisema.

Alisema kutokana na mpangilio wa tafiti za HBS, utafiti mwingine unategemewa kufanyika mwaka 2023/24 hivyo basi anategemea kuona kiwango hicho kinapungua kwa kasi zaidi kwenye utafiti huo ujao.

DK. CHUWA

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa alisema kwa kiasi kikubwa juhudi zinafanyika kupunguza hali ya umasikini na kwamba takwimu zinaonyesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopunguza suala hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Dodoma jana, naye, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Bella Bird alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kueleza kuwa ni sekta ambayo ineweza kuleta mapinduzi nchini.

Alisema ni lazima iwekeze kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa kama imejidhatiti kufikia uchumi wa kati.

“Nimekuwa nikitembea na kukutana na vijana wakanieleza ni namna gani sekta ya kilimo hususani kilimo biashara imeokoa maisha yao hivyo ni muhimu kila nchi iwekeze kwenye kilimo maana zina vijana wengi,”alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya NBS Dk. Amina Msengwa alisema  ripoti hiyo ni   muhimu na  itasaidia kutoa mwongozo kwa Serikali kufuatilia mipango ya nchi katika mambo mbalimbali.

 “Kwa sasa tumesimamia asilimia 26.4 kiwango hicho hatutegemei kujirudie tena kwa hiyo kitazidi kushuka,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles