29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bei ya kuunganishiwa umeme Dodoma ni shilingi 27,000 tu

Na Zuena Msuya, Dodoma

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema kuwa, kuanzia leo maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma yataunganishiwa umeme kwa gharama ya Sh 27,000 tu na si zaidi ya hapo.

Dk. Kalemani amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ya mitaa ya Mkoa wa Dodoma ikiwemo iliyopo katika Kata ya Ntyuka iliyofanyika Aprili 01, 2021.

“Nimefanya ziara ya kujiridhisha kuona kwa nini wananchi wengi hawaunganishi umeme,nikagundua kuwa moja ya sababu ni bei kubwa ya kuunganisha umeme, na maeneo mengi ya makazi ya Dodoma ni kama vijiji hivyo, mradi wa usambazaji wa umeme vijijini ulikuwa katika mkoa huu hata kabla ya kuwa Makao Makuu ya nchi, hivyo naagiza wakandarasi pamoja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha wakazi wa mkoa huu wote wanaunganishiwa umeme Sh 27,000, pasipo kuruka nyumba wala kuzibagua,” alisema Kalemani.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (pili kushoto) akizungumza, wakazi wa Kata ya Ntyuka wakati Waziri wa Nishati alipokuwa akikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kata ya Ntyuka jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde (pili kushoto), iliyofanyika Aprili 01, 2021

Kwa mantiki hiyo, amewataka wananchi wote ambao wametandaza nyaya katika nyumba zao kulipia gharama hizo haraka iwezekanavyo ili kuunganishiwa umeme.

Ameeleza kuwa, awali baadhi ya maeneo ya Mji wa Dodoma yalikuwa yakiunganishiwa umeme kwa zaidi ya shilingi laki tatu.

Aidha, ameagiza kuwa, transfoma ziongezwe kwenye maeneo mbalimbali nchini kwani inapofungwa transfoma moja katika eneo lenye makazi mengi, inapelekea umeme kukatika mara kwa mara.

Kuhusu utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa TANESCO la kuunganishia umeme wananchi wote waliolipia huduma hiyo, amesema kuwa bado siku 14 tu za kufikia ukomo wa agizo husika na hatua zitachukuliwa kwa watendaji wa TANESCO ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati amesema kuwa, ukarabati wa mitambo mbalimbali ya umeme nchini umekamilika hivyo hatarajii kuona umeme ukikatika mara kwa mara na kwamba ikiwa kuna Meneja wa Wilaya ambaye katika eneo lake umeme unakatika mara kwa mara, ndani ya siku 15 atatoa maelekezo ya kuwabadilisha Mameneja na wengine kushushwa vyeo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiwaonyesha jambo ujumbe alioambatana nao katika ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika Kata ya Ntyuka jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde (kushoto mwenye kofia), na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Jones Olotu (Nyuma ya Mbunge), iliyofanyika Aprili 01, 2021.

Kuhusu umeme Vijijini, alieleza kuwa, wananchi ambao bado hawajasambaziwa umeme, watapata nishati hiyo ndani ya miezi 18 na wakandarasi wameshaanza kazi hiyo kutoka Machi 15, 2021. Pia vitongoji navyo vimeshaanza kusambaziwa umeme na kazi husika itakamilika ndani ya miaka Miwili.

Vilevile ametoa msisitizo wa watendaji husika kuwa hataki kuona nguzo za umeme zimelala chini na badala yake zisimikwe katika maeneo yanayohitaji nguzo hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles