Na ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM
MTU mmoja amefariki dunia na wengine 43 wamejeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea eneo la Kamata Kariakoo, Dar es Salaam juzi usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Ilala, Salum Hamduni, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 usiku wakati treni hiyo ikitokea Stesheni kwenda Ubungo.
Alisema treni hiyo ilipofika katika Kituo cha Kamata Kariakoo, basi namba T 696 CVB mali ya Kampuni ya UDA liliigonga na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi hao.
“Dereva wa basi hilo alisimamishwa na mtu aliyekuwa akitoa ishara kwamba asipite kwa sababu treni ilikuwa karibu, lakini alikiuka agizo hilo na kupita, ndipo ajali hiyo ikatokea.
“Tunaendelea kumshikilia dereva wa basi hilo kwa mahojiano na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Hamduni.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na majeruhi wanaendelea kutibiwa hospitalini hapo.
Kamanda Hamduni aliwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka matatizo kama hayo ambayo yanasababishwa na uzembe.