28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe abeba maeneo saba ya bajeti

pG 2Na Kulwa Mzee, Dodoma

MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), leo anatarajia kuwasilisha mapendekezo ya sheria ya fedha katika maeneo saba ya kodi katika bajeti ya mwaka 2016/17.

Katika mapendekezo hayo, Bashe ameainisha vyanzo vipya vitatu vya mapato ili kufidia marekebisho aliyopendekeza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana katika viwanja vya Bunge, Bashe aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni mabadiliko ya ongezeko la kodi katika magari na bodaboda.

Alisema  Serikali kwa kuongeza kodi kutoka Sh 150,000 hadi 250,000 kwa magari na Sh 45,000 hadi 95,000 kwa bodaboda, inatarajia kupata Sh bilioni 21 kwa mwaka, hivyo anapendekeza isiongezwe ibakie ile ya zamani.

“Nilisema nilipokuwa nachangia bungeni, kwa kuweka kodi ya asilimia 18 kwenye utalii, Serikali inategemea kupata Sh bilioni 51, lakini itasababisha utalii kushuka.

“Katika uwindaji, awali Serikali ilikuwa inakusanya Dola za Marekani milioni 20, hivi sasa inakusanya Dola milioni nne jambo ambalo linaonyesha kushuka kwa sekta hiyo.

Kuhusu tozo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), alisema:“Kutoza kodi katika hisa haisaidii kulikuza soko letu, Kenya wenzetu walilifuta, nimeshauri waanzishe kodi ya mzunguko wa jumla,”alisema.

Akizungumzia kodi ya mitumba, Bashe  alisema imeongezeka kutoka Dola za Marekani 0.2 hadi Dola 0.4 gharama ambazo zinakwenda kumuumiza mtumiaji.

Alisema mitumba imekuwa ikitumika miaka mingi, hivyo hoja kwamba ina madhara ya kiafya haina mashiko kwani vipo vyombo vya kusimamia ubora wa bidhaa nchini, ikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambao watahakikisha inaletwa mitumba isiyo na madhara kwa afya ya binadamu.

Alisema katika sheria ya mawasiliano, Serikali inalazimisha kampuni za simu kujisajili katika Soko la Hisa ndani ya miezi sita,jambo ambalo linaweza kuporomosha mtaji wa kampuni hizo kwa pamoja.

“Sikubaliani na kuwalazimisha kujisajili kwa pamoja ndani ya kipindi cha miezi sita, kufanya hivyo tutashusha thamani ya hizi kampuni… nashauri kila Mtanzania aruhusiwe kuwa na hisa katika kampuni hizi tofauti na ilivyo sasa ambapo Mtanzania mmoja mmoja ndiye ana hisa katika kampuni ya simu,”alisema Bashe.

Kuhusu kodi za miamala ya simu,  alisema Serikali haijasema inaweza kudhibiti vipi gharama zitakazobebwa na mtumiaji wa mwisho.

Kwa upande wa msamaha wa kodi kwa mazao yasiyosindikwa, Bashe  alisema Serikali inamaanisha yakishasindikwa watayadai kodi jambo ambalo linarudisha nyuma wajasiliamali wa ndani.

“Maoni yangu ili kukuza viwanda vyetu, Serikali ifute kodi kwa mazao yaliyosindikwa na yasiyosindikwa,”alisema.

Ili kupanua wigo wa mapato ya serikali, Bashe alipendekeza vyanzo vitatu vya mapato ambavyo ni uvuvi katika bahari kuu, ambapo zikipatikana kampuni kubwa Serikali inaweza  kupata zaidi ya Sh bilioni 200 kwa mwaka.

Eneo jingine, alilitaja ni Serikali kuweka utaratibu na sera kwa kuruhusu soko la kuuza na kununua madini kwa kutoza kodi chini ya asilimia moja kwa wafanyabiashara wa nje watakaokuja kuuza madini yao nchini.

Alipendekeza Serikali ipeleke muswada huo katika Bunge la Septemba, mwaka huu  ili utungiwe sheria.

Leo Bunge linapiga kura kupitisha bajeti ya mwaka 2016/2017 na kesho Sheria ya Mabadiliko ya Fedha itajadiliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles