21.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari ya Kabwe kufungua milango ya kiuchumi

ESTHER MBUSSI- RUKWA

Wakazi wa Mkoa wa Rukwa, watafaidika kibiashara na usafiri wa maji kutokana Bandari mpya ya Kabwe, iliyopo mkoani hapa inayotarajia kukamilika Aprili mwakani.

Bandari hiyo ya kisasa inayojengwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) na kugharimu Sh bilioni 7.498 ambazo ni fedha za ndani,

inatarajiwa kufungua milango ya kiuchumi na biashara hususani  ya mazao ya chakula baina ya nchi za Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia.

Wananchi wa mkoa huo, wanaoishi jirani na maeneo ya Ziwa Tanganyika, wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakisafirisha mazao kama mchele, mahindi, maharage, unga na sukari kwenda nchi hizo kwa kutumia mitumbwi lakini baada ya ujenzi wa bandari hiyo kukalimika watasafirisha kwa kutumia meli.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, alisema ujenzi wa bandari hiyo umefikia asilimia 50.

“Mradi huu unajumuisha gati la kisasa lenye kina kirefu, jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ghala la kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio, barabara na maegesho ya magari unaotekelezwa na Mkandarasi Sumry’s Enterprises Ltd kwa gharama za TPA,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Msese alisema mbali na miradi hiyo pia wamejenga ofisi za taasisi za Serikali katika bandari hiyo na zote nchini ili kudhibiti uingiaji wa bidhaa bandia na wahamiaji haramu.

Alisema mamlaka ya Bandari inafanya kazi na Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ili kudhibiti uhalifu katika mipaka hiyo.

Naye mmoja wa wafanya kazi za ujenzi katika bandari hiyo, Ally Rashid, alisema anaishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umemsaidia kupata ajira ya muda na kuweza kujikimu kimaisha.

Kwa upande wake mfanyabishara wa kusafirisha mizigo kutoka Kabwe kwenda Kigoma na nchi za Congo na Burundi, Mohamed Nasoro, aliipongeza TPA kwa kuanzisha mradi huo na kusema kuwa utasaidia kupunguza adha walizokuwa wanapata za kusafirisha mizigo michache kwenda katika nchi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles