ESTHER MBUSSI-CHATO
BANDARI ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato mkoani Geita, inatarajiwa kukamilika Agosti 23, mwaka huu.
Mradi wa ujenzi huo uliogharimu Sh bilioni 4.1 ambazo ni fedha za serikali, unajengwa na Mkandarasi wa ndani ambaye ni Kampuni ya VJ Mistry, kutoka Bukoba mkoani Kagera.
Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina, akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo jana, alisema mradi huo unaendelea na uko katika hatua ya asilimia 40 utekelezaji.
Alisema sehemu ya kazi iliyobakia ni kumalizia ujenzi wa gati, jingo la abiria, jingo la mizigo, chumba cha mashine ya umeme, vyoo na chumba cha walinzi.
“Katika gati hili, meli ziliacha kuja miaka minane iliyopita kwa sababu kampuni iliyokuwa inaleta meli hizo kusitisha kwa sababu zao wenyewe lakini Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) wameurudisha mradi huu,” alisema.
Msina alisema bandari hiyo itakapoanza kazi itachochea biashara kati ya nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na nchi jirani. Naye mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo, Injinia Anderson Mbogowe alisema hadi jana mradi huo umefikia asilimia 47.