33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Utata wagubika kifo kigogo wa polisi

  • Mwili wake wakutwa nje ya nyumba yake, Kamishna wa Polisi atoa neno

KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR

UTATA mkubwa umegubika kifo cha aliyekuwa Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi (DCP), Aziz Juma Mohamed, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maadhimisho makao makuu ya jeshi hilo.

DCP Aziz alikutwa amejinyonga nje ya nyumba yake huko Kibweni, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akizungumza jana baada ya mazishi, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohammed Haji Hassan, alisema kifo hicho si cha kawaida na tayari wameanza kufanya uchunguzi.

“Si jambo la kawaida kuona askari akifa katika mazingira yenye utata, si suala zuri na jema kuona vifo vya aina hii vikitokea kwa watendaji wa Jeshi la Polisi huku sababu ikishindwa kujulikana.

“Tunapata wasiwasi mkubwa sana kuhusu vifo vya aina hii, vinatuweka katika wakati mgumu ambao bado unazidi kutupa mashaka,” alisema Kamishna Hassan.

Alisema Jeshi la Polisi limepata pengo kubwa kutokana na mchango aliokuwa nao marehemu wakati wa uhai wake.

Kwa mujibu wa kamishna huyo, mbali ya kufanya kazi zake za kawaida, DCP Aziz pia alikuwa mwalimu wa jeshi hilo.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alisema jeshi limepoteza kamanda ambaye ni tegemeo kwa wananchi na taifa.

Mazishi yake yalihudhuriwa na wananchi, Jeshi la Polisi, viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa akiwemo pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed.

Marehemu ameacha wajane wawili na watoto watano.

WASIFU

Akisoma wasifu wa marehemu, Naibu Kamishna wa jeshi hilo, Kamwele, alisema alizaliwa Machi 7, 1960 kijijini kwao Michakaeni Chake Chake, Pemba.

Alisema alipata elimu ya msingi na sekondari katika Shule ya Madungu mwaka 1977, na mwaka 1978 alikamilisha elimu ya sekondari katika Shule ya Fidel Castro iliyopo Wilaya ya Chake Chake ,Mkoa wa Kusini Pemba.

Mwaka 1979 alipata Cheti cha Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwaka 2016 alipata Stashahada ya Elimu ya Usalama katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa kilichopo Dar es Salaam.

Mwaka 2002 alishiriki mafunzo ya makosa ya jinai katika Chuo cha Almubaraak nchini Misri.

Pamoja na na mambo mengine, wakati wa uhai wake aliwahi kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuwahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

 Julai 16, 2016 Rais Dk. John Magufuli alimpandisha cheo kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).

Hadi mauti yanamkuta, alikuwa Mkuu wa Kamati ya Mapambo na Sherehe za Kitaifa Jeshi la Polisi Tanzania.

MATUKIO MENGINE

Oktoba 13, 2012, aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Liberatus Barlow, aliuawa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza.

Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo, Said Mwema, alisema tukio hilo lilitokea wakati kamanda huyo akitoka kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la Frolida Hotel Mwanza mjini, akiwa na ndugu yake waliyeongozana naye kutoka kwenye kikao hicho. 

Alisema wakati akimshusha ndugu yake eneo la Kitangiri Minazi Mitatu, walitokea watu wanaosadikika kuwa ni majambazi na kumvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi kisha kumuua papo hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles