28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bajeti ya Serikali yapita

Na RAMADHAN HASSAN-DOOMA

BAJETI Kuu ya Serikali ya Sh trilioni 33.1 kwa mwaka 2019/20 imepita huku mawaziri wakitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge kwa siku saba wakati wakichangia mjadala huo. 

TAULO ZA KIKE

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alitumia dakika 50 kujibu hoja za wabunge kwa muda wa dakika  50 huku akisisitiza  dhamira ya Serikali  kuhakikisha taulo za kike zinapatikana  kwa bei nafuu.

Dk. Mpango alisema Serikali imetafakari  juu ya mapendekezo ya wabunge kuhusu hitaji la taulo za kike  na kwamba jambo hilo ni muhimu.

“La kwanza ni kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni kwenye sheria ya kodi ya mapato kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020/2021 kwa wawekezaji wapya na viwanda vilivyopo vinavyozalisha taulo za kike hapa nchini.

“Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa hii bidhaa muhimu sana, lakini pia kuongeza ajira na mapato ya Serikali. 

“Kwa kuwa hatua ya uwekezaji inaweza kuchukua muda kiasi na ni nia ya Serikali kuhakikisha hatua hii inaleta manufaa kwa haraka, Serikali pia imeamua kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili.

“Jambo jingine itaongeza matumizi ya pamba hapa nchini, lakini pia ajira, na hii ni pamoja na hatua nyingine ambazo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (Kijaji) amezieleza kwa maana ya ujenzi wa kiwanda kimoja na MSD na kingine kule Simiyu kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hiyo muhimu kwa ajili ya watoto wetu wa kike na akina mama.

“Hatua ya tatu inabaki ile ile, kwamba tunafuta msamaha wa VAT uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike kwa kushindwa kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake kuwanufaisha wafanyabiashara.

“Kwa kweli lengo la Serikali ni kumnufaisha mtoto wa kike na sio wafanyabiashara kujilimbikizia faida, napenda kusisitiza kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba bidhaa hiyo muhimu inapatikana kwa bei nafuu na hivyo kuwawezesha watoto wa kike na wanawake kuinunua.

“Kwa msingi huo, tutaingia mkataba wa makubaliano, yaani ‘performance agreement’ na kila mwekezaji atakayenufaika na punguzo hili la kodi ya mapato ambayo itaainisha wajibu wa kila upande. Lakini sasa Serikali itafuatilia mwenendo wa bei za hizo taulo za kike,” alisema.

Kuhusu hoja ya Serikali kuboresha masilahi ya watumishi wa umma, Dk. Mpango alisema jambo hilo sio la kweli.

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipunguza kodi katika mishahara (PAYE) kutoka digiti mbili hadi moja.

Aidha hadi kufikia Mei mwaka 2018/19, Serikali imelipa madai mbalimbali ya watumishi jumla ya Sh bilioni 64.97 na pia ilipandisha madaraja watumishi wote waliokuwa wanastahili ambapo jumla ya Sh bilioni 14.55 zilitumika hadi kufikia Mei 2019.

Dk. Mpango alisema ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kupandisha mishahara ya watumishi wa umma iko pale pale.

“Naomba niwataarifu wabunge Serikali katika hili tumekuwa tukifanya maboresho ya mfumo wa kodi, tozo na ada mbalimbali ili kuongeza mapato, kuboresha mazingira ya kufanya biashara, lakini pia mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii yanayoguswa na mfumo huo,” alisema Dk. Mpango.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alisema Serikali itajenga viwanda vya kuzalisha taulo za kike kama hatua ya kumwezesha mwanamke kupata bidhaa hiyo muhimu.

Alisema viwanda hivyo ujenzi wake utaanza mwaka huu ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), utajenga kiwanda cha taulo za kike mkoani Simiyu.

Dk. Kijaji alisema kiwanda kingine kitajengwa mkoani Pwani na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambapo vyote zitauza bidhaa hiyo kwa bei rahisi.

“Kufutwa VAT kwenye taulo za kike, mimi ni mwanamke na nina mchango wangu kwa kila kinacholetwa na Waziri wa Fedha. Naijua kadhia hii haipendezi hata kidogo kwa maneno aliyoelezwa kwa Waziri wa Fedha kwenye Bunge hili.

“Anapoleta hoja huwa ya Serikali na sio yake, tusimshambulie naye ni binadamu anaumia.

“Watu wanasema bajeti haina misingi ya kijinsia. Nimefanya mapinduzi makubwa kwa afya ya wanawake. Tumepeleka Simiyu Sh bilioni 4.5 kujenga hospitali kwenye halmashauri zake ili wanawake wapate huduma za afya. Tumepeleka Geita Sh bilioni tatu kwa mwaka mmoja. Kanda yote ya ziwa tumepelekwa Sh bilioni 22,” alieleza.

Naibu waziri huyo alibainisha kuwa baada ya kuondoa kodi ya VAT kwenye taulo za kike, Serikali ilifanya utafiti kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Alisema hawezi kuvumilia kuona wafanyabiashara wanashirikiana na watumishi wa Serikali kukwepa kodi.

Kijaji alisema Mei hadi Aprili mwaka huu, zaidi ya watumishi 30 wa TRA wamesimamishwa kazi. 

“Aprili 19 mwaka huu, nilipokea vijana watatu ofisini kwangu kulalamika wamepewa makadirio makubwa ya kodi. Nilipoanza kuifuatilia ilikuwa malori manne ya tani 10 yaliyobeba vitenge kutoka China. 

“Yamepita bandari ya Dar es Salaam, kwenda Uganda ambapo yalionekana yamepita kwenye mpaka wa Mtukula, lakini hawakuwa na nyaraka kuonyesha kama yametokaje Uganda. 

“Nilichokibaini, waliokuja wale vijana walikuwa madalali wakishirikiana na maofisa wa TRA, waliokusanya kodi halali kutoka kwa wafanyabiashara. Kama hilo ndio linalotafsiriwa Ashantu (Kijaji) anasimamia kufungwa biashara. Sitaruhusu Watanzania waibiwe. Nitahakikisha kodi zinakusanywa kulingana na sheria zilizopitishwa na Bunge,” alisema.

JAFO NA VITAMBULISHO

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ametoa ufafanuzi kuhusu vitambulisho vya wajasiriamali.

Jafo alisema mjasiriamali anayepaswa kupewa kitambulisho ni lazima awe anatengeneza kipato cha chini ya Sh milioni 4 kwa mwaka.

Alisema kuna baadhi ya mikoa maelekezo hayo yametafsiriwa vibaya na ndiyo sababu ya kuibuka kwa changamoto ambazo wameanza kuzifanyia kazi.

Kuhusu bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kutotosha, Jafo alisema Serikali imeanza kuchukua hatua.

“Ni kweli bajeti ni ndogo, lakini fedha zaidi ya Sh bilioni 284.7 zimetengwa kuboresha miundombuni ya barabara. Pia bodi ya barabara inaangalia kanuni ya 30/70 kuangalia namna barabara za Tarura zitakavyoweza kuboreshwa,” alisema.

Alisema Sh bilioni 58.24 zimetengwa kwa shule za sekondari kuboresha miundombuni ya elimu.
Aidha, kwenye sekta ya afya  alisema Serikali imefanya kazi kubwa ambapo kwa mwaka huu vituo vya afya 52 na hospitali mpya 27 zinajengwa. 

“Ndani ya miaka miwili hospitali 94 zitakuwa zimejengwa, wakati tangu uhuru hadi mwaka 2015 tulikuwa na hospitali 77, lakini ndani ya miaka miwili hospitali mpya 94 zimejengwa, tumevunja rekodi ambayo haijawahi kutegemewa,” alisema.

MAKAMBA NA MUUNGANO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba, alisema namna muungano ulivyozungumziwa kwenye michango ya baadhi ya wabunge kuna maneno yaliyojenga na kubomoa.

Alisema baadhi ya lugha zilizotumika hazichangii kujenga muungano kwani zimetuhumu, kutusi na kuleta fedheha kubwa. 

“Naomba kwa heshima ya bunge na nchi, kwa dhana ya kuhimiza umoja na mshikamano, imefika mahali maneno ya aina hiyo yasitumike katika Bunge letu.

“Baadhi ya michango imedai kunukuu bajeti iliyosomwa Zanzibar, kuwa Waziri Mpango na Serikali ya Tanzania ina roho mbaya, wivu na chuki kwa Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar, kugoma kutekeleza mambo ya maendeleo ya Zanzibar.

“Hayo maneneo kama yalivyonukuliwa kuwa yalisemwa kwenye bajeti ya Zanzibar, si kweli, kwani nilikuwepo wakati bajeti hiyo ikisomwa, ilisomwa kwa staha na umakini. Tusiwatie maneno viongozi wa Zanzibar, kujenga hoja ya maeneo yenye kutaka kuvuruga muungano,” alisema.

Makamba alimwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai, asaidie Bunge lisiwe chanzo cha kuleta ufa nchini.

“Uhodari wa kuunajisi muungano kwa maneno machafu ili kupata umaarufu wa kisiasa, tusikubali. Tunakubali Serikali ya Zanzibar ina bajeti yake, mpango wa maendeleo na Ilani ya chama.

Mara baada ya Makamba kueleza hayo, Spika Ndugai, alimuunga mkono akisema Bunge litaongeza umakini kufuatilia michango ya aina hiyo yenye lengo la kuhatarisha muungano.

“Naungana na wewe, hatutaruhusu Bunge kuwa sehemu ya kuanzisha cheche zitakazowasha moto kuunguza nchi yetu. Tutaongeza umakini kufuatilia na kusikiliza kuhakikisha mambo hayo hayatokei tena. Bila Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata Bunge halitokuwepo. Kazi yetu ni kulinda,” alisema.

BASHUNGWA NA KOROSHO

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, alisema katika soko la korosho kumekuwa na upotoshaji mkubwa ambao umesababisha dunia kujua kwamba korosho ya Tanzania haifai. 

“Baada ya kuapishwa, nimetembea na kwenda ghala kwa ghala, korosho yetu iko katika hali nzuri, naomba wabunge tuweke uzalendo na utaifa mbele. Hakuna korosho ambayo iko ‘reject’, korosho ni ‘grade one’ na ‘grade two’. 

“Sasa tunapowasiliana na wanunuzi duniani, bado wameendelea kupotosha kwamba korosho sio safi. Tutoe hii korosho kwakuwa mwaka ujao tumejipanga kuwasaidia wakulima wetu,” alisema.

MPINA NA TOZO ZA UVUVI

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Luhaga Mpina, alisema tozo nyingi za mifugo zimeshughulikiwa wakati tozo za uvuvi hazijaweza kushugulikiwa. 

 “Ukija kwenye suala la tozo ni kwanini iwe kwenye uvuvi, ni kweli kabisa kwamba dagaa walikuwa wanatozwa dola 1.5. Sasa nataka niwaambie hivi, tumerekebisha, Serikali imesikia kilio cha wavuvi na imekubali pia ushauri wa wabunge, tumepunguza kodi kutoka 0.5 mpaka 0.3,” alisema Mpina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles