24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Rostam kuwekeza Sh bilioni 500

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya usambazaji gesi ya Taifa Gas, Rostam Azizi amesema wanatarajia kuweka zaidi ya Sh bilioni 500 katika miradi mbalimbali ili kuongeza fursa za ajira na mapato serikalini.

Taifa Gas ambayo awali ilijulikana kama Mihan Gas, inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 iliandikishwa mwaka 2005 na kuanza kufanya biashara mwaka 2008.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa ghala na mitambo ya kampuni hiyo iliyopo katika eneo la Kigamboni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Rostam Azizi, alisema wamevutiwa zaidi kuwekeza kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufanya biashara nchini.

“Tuna kila sababu ya kukushukuru mheshimiwa rais na Serikali kwa kujenga misingi imara na uwanja sawa wa kibiashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Mafanikio tuliyoanza kuyaona ni matokeo ya kazi uliyofanya kwa weledi mkubwa tangu ulipoingia Ikulu mwaka 2015, wewe siyo tu mtetezi wa kweli wa Watanzania wanyonge, bali pia ni rafiki mkubwa wa sekta binafsi.

“Umetambua vema uhusiano wa sekta binafsi utatekelezwa katika uwanja ulio sawa na kuzaa kodi na ajira zitakazosaidia kuimarisha huduma za jamii na miundombinu,” alisema Rostam.

Alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali zimesaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuwavutia wawekezaji wengi, wakiwemo Watanzania waliokuwa wamewekeza nje na kuamua kurudi nchini.

 “Historia itakukumbuka katika hili, msimamo wako thabiti dhidi ya matendo ya ujanja ujanja katika biashara na uwekezaji umetufanya kupata moyo wa kurejesha mitaji yetu nchini na kuwekeza,” alisema.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini kwani milango ya uwekezaji iko wazi, lakini akasisitiza wafanye biashara kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hamis Ramadhani, alisema uwekezaji huo umegharimu Sh bilioni 150 na umetoa ajira kwa vijana 260 wakiwemo wahitimu 130 wa elimu ya juu na ajira zisizo za moja kwa moja 3,500.

Alisema gesi hiyo ya LPG ambayo inatokana na usafishaji wa mafuta ghafi, ni rahisi kusambazwa katika mitungi na kwamba hadi sasa wameshasambaza mitungi milioni moja ya ujazo kati ya kilo tatu hadi 38.

“Tunaunga mkono azma ya kujenga Tanzania mpya ili kulinda rasilimali za nchi, mazingira na kuongeza ajira. Faida ya hatua ulizochukua ndani ya uongozi wako (Rais John Magufuli) ni huu uwekezaji mkubwa tuliofanya na tunatarajia tutakuza soko kwa asilimia 50,” alisema Ramadhani.

Hata hivyo, alisema matumizi ya gesi nchini bado yako chini kulinganisha na nchi nyingine, hivyo kunahitajika uwekezaji mkubwa sambamba na elimu kwa wananchi kuhusu nishati hiyo.

Alisema wananchi wengi bado wanatumia mkaa ambapo kwa wastani familia moja hutumia zaidi ya gunia moja kwa mwezi na kugharimu Sh 90,000 wakati gesi inagharimu kati ya Sh 45,000 hadi 50,000 na wengi wana uwezo wa kumudu.

 “Tunafanya biashara zaidi nje ya nchi, kama Kenya tunawauzia tani 2,000 kwa mwezi, pia tunauza Sudan, Burundi na Congo na hivi sasa tunakamilisha usajili Zambia na Afrika Kusini,” alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wanatarajia kuongeza maghala na mitambo ya gesi, maroli zaidi ya 100 ili kusambaza gesi wilaya mbalimbali nchini na kusambaza mitungi milioni tano.

Mkurugenzi huyo alisema pia wameingia ubia na kampuni ya nchini Japan ili kusaidia kusambaza gesi nje ya nchi na kwamba bado wana mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kwa sasa wanahitaji ekari 15.

CHANGAMOTO

Aliiomba Serikali kuangalia upya utaratibu ambao inataka kuutumia wa kudhibiti soko kwa uagizaji wa pamoja na upangaji wa bei.

Alisema udhibiti unatakiwa uwe kwenye viwango, ufundi na usalama, lakini suala la bei liachwe kuwa huru kwa sababu sekta hiyo bado ni changa.

Alitolea mfano wa Afrika Kusini ambayo ilianza udhibiti tangu mwaka 2010 na tangu wakati huo hadi sasa sekta hiyo imedumaa.

“Udhibiti ambao Serikali inataka kuufanya utaondoa ushindani uliopo na ubunifu katika kukuza soko. Una athari za kimtaji, upangaji bei wa sisi wenyewe umesaidia kuwa na ushindani sokoni.

“Tunakuomba (Rais Magufuli) utusaidie sekta iwe huru kuruhusu ushindani unaochochea uwekezaji wa gharama nafuu,” alisema Ramadhani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles