NA TIMOTHY ITEMBE
MTU Mmoja ambaye jina lake halikufahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30-35 ameuawa kwa risasi na polisi baada ya kuingia katika benki ya NBC usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, alisema mtu huyo aliingia ndani ya benki ya NBC kwa kupitia kwenye tundu lililoko karibu na ATM.
Alisema Agosti 19, mwaka huu saa 6:04 usiku mtu huyo ambaye hajafahamika jina wala makazi yake alifariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi waliokuwa kwenye lindo katika benki hiyo baada ya kumtaka kujisalimisha na kukaidi amri hiyo.
“Mtu huyo alifanya matukio mawili ya kushangaza kwa siku tofauti katika benki hiyo.
“Tukio la kwanza Agosti 18, mwaka huu kati ya saa 4.00 na 6.00 usiku aliingia na kufanikiwa kutoka ndani ya benki bila kuonekana na hakuchukua chochote.
“Tukio la siku ya pili Agosti 19, mwaka huu saa 6:04 usiku aliingia na askari waliokuwa katika lindo waligundua wakati king’ora cha benki kikipiga kelele.
“Baada ya kelele askari walimtaka mtu huyo kujisalimisha lakini alikaidi na kuanza kukimbia.
“Polisi walifyatua risasi ya hewani kumtishia lakini hakusimama walifyatua risasi ya pili ambayo ilimpata na kumjeruhi mguuni na shingoni na kuanguka chini.
“Walimuchukua na kumkimbiza katika hospitali ya wilaya katika jitihada hizo marehemu alifariki akiwa njiani kabla hajafikishwa hospitalini,” alisema Mwaibambe.
Mwaibambe amewataka wakazi wote wa Tarime na Rorya kutoa taarifa wanapokuwa na shaka na mtu yeyote ambaye ana mazingira ya uhalifu.