27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

TAHARIRI: KAMATAKAMATA YA WABUNGE IANGALIWE UPYA

TUMEPATA kuandika mara nyingi kuhusu  kamatakamata ya wabunge.

Leo tumelazimika kurudia kuandikia jambo hili, ili mamlaka zinazohusika zijitafakari.

Mara nyingi tumeandika na kuziasa mamlaka zinazohusika kuwa jambo hili, limekuwa likileta sura mpya ambazo zinazua maswali mengi mbele ya jamii.

Miaka nenda rudi Watanzania walizoea kuishi kama ndugu au familia moja, licha ya kuwapo na tofauti za hapa na pale ambazo siku zote hazijawahi kuwawekea mipaka.

Hali hiyo imedumu tangu Taifa hili linapata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1961. Kila mmoja wetu ni shahidi umoja wa aina hiyo ulivyoweza kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa, dini wala kabila.

Katika siku za karibuni tumeshutushwa na mwenendo wa vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi kukamata wabunge hasa wa upinzani kwa kosa la kutoka jimbo moja kwenda jimbo jingine.

Hapa tunaona kuna kasaro kubwa, tunaamini polisi kama chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia usalama wa raia, wanatambua wazi kuwa wabunge wamechaguliwa kihalali na wananchi kwenye majimbo yao na hawana kinga ya kisheria ya kuzuiliwa kwenda jimbo jingine.

Lakini ndani ya kipindi kifupi, tumeanza kuona sasa hali ya mbunge moja kwenda sehemu nyingine imekuwa ni kosa.

Tumelazimika kusema haya, baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya kumkamata Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya (Chadema) na kuwekwa mahabusu eti kwa kosa la kuhutubia mkutano wa kisiasa nje ya jimbo lake bila kibali.

Suala hili haliingii akilini hata kidogo, hivi  ni kweli Tanzania ya leo ambayo inajinasibu gwiji wa demokrasia Afrika na duniani imefikia hatua hii?

Tunajiuliza bila kupata majibu kwamba, hivi mbunge wa chama fulani kutoka mkoa ule ule anaoishi kwenda kumtembelea mbunge mwenzake tena kwa nia njema ya kwenda kutoa msaada wa mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule ni kosa?

Tunasema hivyo kwa sababu matendo haya yakiachiwa yaendelee kwa kweli yatasababisha mvurugano au chuki zisizokuwa za msingi.

Tuaamini wabunge kupitia umoja wao au vyama vyao wanashirikiana katika mambo mengi tu ya msingi, ikiwamo kutoa misaada ya kijamii katika maeneo yao yenye shida fulani.

Kukamatwa kwa Bulaya na kuwekwa mahabusu, tunaona kama kunafungua sura nyingine ambayo Watanzania kamwe hawakuizoea hata kidogo. Haiwezekani leo mbunge ashindwe kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa nia njema halafu aishie kulala mahabusu.

Katika jambo hili tunalishauri Jeshi la Polisi kujiangalia upya hata kama wanatekeleza maagizo ya ngazi za juu. Wanapaswa kujiuliza ni sheria gani hiyo ambayo inawapa mamlaka hayo.

Siku zote polisi wamekuwa wakifanya kazi nzuri na yenye tija mbele ya jamii, kwanini katika hili wanashindwa kujitafakari?

Hatupendi kuona tunakuwa na Taifa lenye kugawanyika eti huyu yuko kanda ile abaki kule kule, hapana sisi ni ndugu wanafamilia moja.

Sisi MTANZANIA, tunasema vitendo vya aina hii vikiachwa vikaendelea vinaweza kuligawa Taifa kwa ubaguzi wa kisiasa miongoni mwa jamii kwa sababu Watanzania hawakuzoea hili.

Tunamalizia kwa kumshauri pia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kutoa maelekezo ya kina juu ya askari wake wakati mwingine kuwa makini na magizo wanayopewa na wanasiasa au viongozi walio juu yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles