32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

ATAMANI KUIKIMBIA FAMILIA KUKWEPA UKATILI WA MKEWE

 

Na MANENO SELANYIKA, LINDI


UKATILI wa kijinsia ni kitendo kinachofanywa dhidi ya jinsia na kusababisha madhara, maumivu, mateso ya kimwili au kisaikolojia kwa mtu.

Hali hiyo huambatana pia na vitendo vya kutishia au kulazimisha kumnyima mtu uhuru bila kujali vinafanyika kisiri au kwenye kadamnasi.
Ukatili wa kijinsia unahusishwa na ukatili kwa wanawake kwa kuwa wao ndiyo waathirika wakubwa.

Kwa miaka mingi, tumezoea kusikia matukio ya ukatili wa kijinsia wakifanyiwa wanawake na waume au wapenzi wao wa karibu.

Hivyo, kumekuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wanawake wakidai kunyanyasika kwa vipigo na kujeruhiwa na aidha waume au wapenzi wao.

Lakini wapo watu wengine ambao hutelekezwa na familia, kunyimwa haki za msingi kama kumiliki ardhi, kitu ambacho ni kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uchunguzi unaonesha zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia nchini, hushindwa kutoa taarifa kwenye vyombo sheria.

Hata hivyo, watetezi wa haki ya mwanamke na mtoto kikiwamo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na vyombo vya habari vingine, wamekuwa wakifichua hali hiyo jambo lililosaidia kukuza uelewa kwa kiasi kikubwa.

Hivi majuzi, mwandishi wa makala haya alifanikiwa kufika katika Mkoa wa Lindi wilayani Ruangwa, alikobaini kuwa baadhi ya wanaume nao hufanyiwa ukatili wa kipigo na wake zao, tena hupigwa kwa kutumia silaha za aina mbalimbali kama kisu, panga, kuwang’ata na ukatili mwingine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanaume hao kutoka Kata za Wilaya ya Nachingwea na Ruangwa, wanasema kwa muda mrefu wananyanyaswa na wake zao.

Kutokana na hali hiyo, wengine wameamua kukimbia nyumba na kutelekeza familia kwa mambo wanayofanyiwa na wenzi wao ikiwamo kunyimwa tendo la ndoa, kipigo na kutopewa chakula.

Mkazi wa Kijiji cha Keko, Kata ya Nachingwea, Yusuph Chipate anasema yupo katika ndoa kwa miaka saba sasa na mkewe aitwaye Zainab, waliyejaaliwa kupata watoto wawili.

“Huyu mwanamke wakati naanza kumchumbia wazee kule kijijini walinishauri nimuache, walidai ukoo wake ni wa watu wasio na busara, lakini kwa kuwa lilikuwa chaguo langu nikapuuza mawazo yao, nimevumilia mateso sasa nimeshindwa natamani kuhama hapa nyumbani nikatafute sehemu nyingine ya kwenda kuishi,” anasema Chipate.

Anasema mwanamke huyo ni mkazi wa Kijiji cha Mwakanjiro, Kata ya Ruangwa ambaye alimuoa akiwa tayari ana mtoto mwingine aliyezaa kabla ya kufunga naye ndoa.

“Yaani huyu mwanamke najuta kuishi naye ni mcharuko vibaya, wakati mwingine akiwa na hasira anachukua silaha kama panga au kisu na kunitishia kunikata.

“Kuna siku sijui kulitokea nini, alikuja akiwa na hasira kisha aliniparamia na kuning’ata sehemu mbalimbali za mwili, nilipata maumivu makali halafu ilikuwa usiku, kesho yake ilibidi niende hospitali kutibiwa vidonda, kwa sasa makovu yamepona,” anasema Chipata.

Anasema kwa kuwa amemzoea mkewe, akiona amebadilika anajihami kwa  kuficha silaha kama visu, mapanga na vitu vingine ili asije akavitumia kumjeruhi.

“Akipandisha hasira huwa anahema kama simba na akipika chakula hali, kitu ambacho kinanipa wasiwasi nashindwa kutambua mwanamke huyo ni wa aina gani na hatumii aina yoyote ya pombe.

“Mwaka jana baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu, nilipeleka malalamiko kwa wajumbe wa kamati zilizoundwa na TAMWA, aliitwa na tukasuluhisha mgogoro,” anasema Chipata.

Chipata anasema bora mkewe angekuwa anasema tatizo liko wapi angeweza kujirekebisha lakini hazungumzi chochote.

 

Zainabu anazungumziaje tuhuma hizo?

Zainabu ambaye ndiye mlalamikiwa, baada ya kuulizwa kwa njia ya simu kuhusu unyanyasaji huo anaomfanyia mumewe kwamba ni viashiria vya ukatili? Alikanusha na akadai haoni sababu ya mumewe kuzungumza na mwandishi wa habari kuhusu masuala ya ndani ya nyumba yao.

“Mimi sina ugomvi na mume wangu, wewe nani alikueleza hizo taarifa? Umeambiwa na jirani au yeye mwenyewe? Kama ni yeye aliyekueleza basi anatakiwa achukue uamuzi badala ya kulalamika serikalini.

“Mimi naishi naye tu, sina ndoa, kama mzigo ameuchoka auweke chini, kwani tulivyokubaliana aliita watu wa serikalini? Iweje leo hii anazungumza masuala kama haya, tena we ngoja nitakuja kumuuliza,” alijibu Zainabu ambaye alionekana kupandwa na hasira.

MTANZANIA lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya majirani wa eneo analoishi Chipata na familia yake, walitoa ushuhuda kuwa ugomvi wao ni wa muda mrefu huku wengi wao wakidai kuwa mwanamke hamuheshimu mumewe, kwani anaweza kufanya jambo lolote bila kumshirikisha.

“Hao kila siku mwanamke anampiga mumewe, sisi hatuwezi kuamua kwa sababu ni ugomvi wa mke na mume wenyewe wanajuana na wanaelewana,” anasema jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama Beka.

Sanga Paul, ni mkazi wa eneo la Keko anasema hivi majuzi alishuhudia jirani yake akimfukuza mumewe kwa sababu ameshindwa kutoa huduma kwa watoto badala yake anakunywa pombe muda wote akipata fedha.

Wanaume wengi wilayani Ruangwa hunyanyaswa na wake zao lakini hawaoni umuhimu wa kutoa taarifa kwenye ngazi mbalimbali ili wapatiwe msaada wa kisheria wa kuweza kutatua adha hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya ofisini kwake, Sajenti Jonas Gaganija wa Dawati la Jinsia Kata ya Ruangwa na Nachingwea, anasema matukio ya ukatili kwa wanaume kutoka kwa wake zao ni mengi lakini yanayoripotiwa ni machahe.

Anatolea mfano wa Oktoba, mwaka huu, hajapokea malalamiko ya aina yoyote ile.

“Tumepokea kesi moja tu ya mwanamume aliyetelekeza familia ila baadaye ile kesi haikuendelea, mlalamikaji aliomba warudi wakayazungumze na familia.

Kwa ujumla malalamiko ya kesi za ukatili wa kijinsia kama ubakaji, ndoa za utotoni, kulawiti, vipigo na nyingine, kwa mwezi tunaweza kupokea kesi kati ya sita hadi 20,” anasema Sajenti Jonas.

 

Mkuu wa wilaya atoa ufafanuzi

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiti anasema familia nyingi wilayani humo, upande wa mama ndiyo wenye nguvu na hutoa uamuzi wa jambo lolote lile la familia hata kama baba yupo ambaye anapaswa kuwa kiongozi wa familia.

“Familia za huku ni zile zinazofuata mfumo wa ‘Matrilenier’ yaani mtoto anapewa jina kutoka upande wa mama, hivyo kadiri siku zinavyozidi kusonga, ndoa nyingi zinavunjika halafu cha ajabu, unaweza kuona wanagawana mali, kitu kama godoro linakatwa katikati…huoni hicho ni kitu cha ajabu?” anasema.

Anasema vitendo vya ukatili katika ngazi ya familia vitakomeshwa tu kama kila kiongozi atakemea tabia hii kwa sauti kuu ili wahusika wasikie na wajirekebishe.

Aidha, binadamu yeyote endapo akifanyiwa vitendo vya ukatili anakuwa na uwezo mdogo wa kufikiri, hali hii itamfanya ashindwe kuzalisha, hivyo uchumi wake hushuka na kujikuta akijiongezea umaskini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles