24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI: MARADHI YA FIZI HUONGEZA HATARI YA SARATANI YA TITI

MARADHI ya fizi huongeza hatari ya kupata saratani ya titi kwa wanawake kwa kiwango hadi mara tatu, utafiti mpya umebainisha.

Hii inadhaniwa kutokana na bakteria wanaosababisha uvimbe mdomoni kuingia katika njia ya usambazaji wa damu kupitia fizi,  kisha kuingia katika tishu za titi, ambazo zinaweza kusababisha saratani.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Dk. Nigel Carter, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Mdomo, Oral Health Foundation anasema: “Kinachovutia zaidi, utafiti huu unaonesha kuna ushahidi wa kuunga mkono nadharia iliyopo kuwa maradhi ya fizi yanaweza kuwa na athari kubwa katika afya ya miili yetu.”

Maradhi makali ya fizi yanayojulikana kwa kitaalamu kama periodontitis, yanaweza kuathiri mifupa katika taya za watu na kusababisha meno kung’oka.

Tafiti za nyuma zilifichua kwamba hadi asilimia 54 ya watu wazima nchini Uingereza wana maradhi ya fizi kwa kiwango fulani.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Santa Maria nchini Brazil walifanya uchambuzi kwa wanawake 201 waliotembelea idara ya jinakolojia (Uzazi) katika Hospitali ya chuo hicho kikuu kati ya Aprili 2013 na Juni 2015.

Kati ya washiriki wa utafiti huo, 67 walikutwa na saratani ya titi.

Kesi na udhibiti vililingana kwa mujibu ya hali ya uvutaji sigara na unywaji pombe. Na washiriki wote walifanyiwa uchunguzi wa uvimbe katika fizi.

Matokeo yakabainisha kwamba maradhi makali ya fizi yana uwezekano wa kuongeza hatari mara tatu kupata saratani ya matiti.

Hata hivyo, utafiti haukuonesha uhusiano wowote baina ya upotevu wa meno na uzalishaji wa maradhi.

Dk. Carter alisema: ‘Kinachovutia ni kwamba utafiti huu unaonesha kuna ushahidi wa kuunga mkono nadharia kuwa maradhi ya fizi yana athari kubwa katika afya za miili yetu.

‘Unaonesha kuwa maradhi makali ya fizi yanahusiana na kesi za saratani ya matiti na hili kutokea kupitia msambao wa uambukizo na uvimbe unaoanzia mdomoni.

Uhusiano huo pia unaonekana kuwa nguvu kwa saratani ya mdomo, lakini pia ulionekana baina ya afya duni ya mdomo na mapafu, matiti na saratani ya ngozi.

Aidha uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe huongeza hatari ya maradhi ya fizi na saratani, hivyo wakati wa utafiti watafiti walitenganisha wale wasiovuta sigara na wavutaji.

Wasiovuta sigara bado walionekana na uwezekano wa mkubwa mara tatu ya kupata maradhi ya saratani iwapo wana maradhi ya fizi.

 

Watafiti hawana uhakika sababu ya maradhi ya fizi na saratani kuwa na uhusiano, anasema mwandishi mwandamizi wa utafiti huo Jean Wactawski-Wende.

Hata hivyo, maradhi ya fizi yanapofikia hatua mbaya ya ‘periodontal’ ambayo humaanisha uvimbe kuzunguka meno kunaweza kusababisha utando ambao vinaweza kuwa sumaku kwa vyakula na bakteria.

Baada ya kipindi fulani, uvimbe na bakteria unaweza kusababisha upotevu wa meno.

Wactawski-Wende na watafiti wenzake wanadhani kwamba bakteria hao katika mashimo mdomoni wanaweza kuwa sababu.

“Virusi hivi vinaweza kusafiri kwenda sehemu tofauti za mwili kupitia mate yako na huungana na tumbo na umio wakati unapomeza au kuishia katika mapafu yako wakati wa upumuaji,” anasema Dk. Wactawski-Wende.

 

Waandishi wa utafiti huo, hata hivyo wanasema kuwa tafiti zaidi zinahitajika ili kutambua uhusiano maalumu’

 

Matokeo yalichapishwa katika jarida la masuala ya afya ya meno na mdomo lijulikanalo kama Community Dentistry and Oral Epidemiology

 

 

Je, unakabiliwa na hatari ya kupata maradhi ya fizi?

 

Ni maradhi ambayo huwapata watu wengi sana ulimwenguni.

Hata hivyo, katika hatua za awali dalili zake hazionekani haraka na hivyo kuwa hatari kwa kuwa hautambuliki mapema.

Kwa mujibu wa Jarida la Kimataifa la Meno, maradhi ya fizi ni kati ya magonjwa ya kinywa yanayosababisha “tatizo kubwa la afya ya umma.”

Linasema kwamba ugonjwa wa kinywa unaweza kusababisha uchungu mwingi na kuteseka na kupunguza uwezo wa mtu wa kula na kufurahia maisha.

 

Ugonjwa wa fizi una hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza ni kuvimba fizi (gingivitis), ambapo fizi kutoa damu ni dalili ya hatua hiyo.

Huenda mtu akatokwa na damu anapopiga mswaki, au anapotoa uchafu kwenye meno kwa kutumia uzi mwembamba au kutoka yenyewe bila sababu yoyote.

 

Vilevile, kutokwa na damu mtu anapochunguzwa meno na daktari ni dalili ya ugonjwa huo.

 

Ugonjwa wa fizi husonga kwenye hatua inayofuata (periodontitis). Kufikia hatua hiyo, mifupa na fizi zinazotegemeza meno, huanza kuharibika.

Dalili fulani za hatua hiyo ni kutokea kwa nafasi kati ya fizi na meno; kulegea kwa meno; mianya kati ya meno; kunuka mdomo; fizi zinazoachana na meno na kufanya meno yaonekane kuwa marefu zaidi; na kutokwa na damu kwenye fizi.

 

Chanzo na madhara ya ugonjwa wa fizi

 

Kuna mambo kadhaa yanayochangia kupata ugonjwa wa fizi. Utando wa bakteria ambao kwa kawaida hutokea kwenye meno ndicho chanzo kikuu.

 

Usipotolewa, bakteria husababisha kuvimba kwa fizi. Hatua hiyo inapoendelea, fizi  huachana na meno, na hivyo utando huo wa bakteria husambaa na kuingia chini ya fizi.

Bakteria zinapofikia hatua hiyo, uvimbe huendelea kuharibu mifupa na fizi. Utando huo, iwe uko juu au chini ya fizi, unaweza kuwa mgumu na kuwa ukoga.

Ukoga pia una bakteria, na kwa kuwa ni mgumu na hushikamana na meno, hauwezi kutolewa kwa urahisi kama utando. Hivyo, bakteria huendelea kuharibu fizi.

 

Kuna mambo mengine pia yanayochangia ugonjwa wa fizi ikiwa ni pamoja na uchafu mdomoni, dawa zinazopunguza kinga mwilini, magonjwa yanayosababishwa na virusi, kisukari, kunywa pombe kupita kiasi, kutumia tumbaku, na mabadiliko ya homoni kwa sababu ya mimba.

 

Ugonjwa wa fizi unaweza kukuathiri kwa njia nyingine pia. Maumivu mdomoni na kung’oka meno kunaweza kupunguza uwezo wako wa kutafuna chakula na kukifurahia.

Pia, unaweza kuathiri matamshi na sura yako. Vilevile utafiti umeonyesha kwamba usafi mdomoni unahusiana na afya ya mtu kwa ujumla.

 

Kutambua na kutibu ugonjwa wa fizi

 

Unawezaje kujua kama una ugonjwa wa fizi? Huenda ukaona baadhi ya dalili zilizotajwa kwenye makala hii. Ukiziona ni vizuri kumwona daktari maalumu wa meno ili achunguze fizi zako.

 

Je, ugonjwa wa fizi unaweza kutibiwa? Inawezekana kuutibu katika hatua za kwanza.

Ugonjwa wa fizi unapoenea sana, basi lengo ni kuuthibiti ili usiendelee kuharibu mifupa na fizi zinazotegemeza meno.

Madaktari wa meno hutumia vifaa vya pekee vinavyoweza kuondoa utando na ukoga kwenye meno, iwe ni chini au juu ya fizi.

 

Hata ikiwa si rahisi kwako kupata matibabu ya meno, unaweza kuzuia ugonjwa huo hatari usikupate. Kusafisha mdomo vizuri na kwa ukawaida ndiyo njia bora zaidi ya kuzuia ugonjwa wa fizi.

 

Usafi mdomoni

 

Piga mswaki angalau mara mbili kwa siku. Huenda watu fulani wakahitaji kupiga mswaki mara nyingi zaidi, labda kila baada ya kula, ili kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa fizi

 

Tumia mswaki ulio laini, na upige mswaki taratibu, na kwa karibu karibu

 

Toa uchafu katikati ya meno kila siku ukitumia uzi mwembamba wa pekee, au ikihitajika mswaki maalumu na vijiti vya kutoa uchafu katikati ya meno

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles