23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NASARASHI SERETI: NYUMBA YANGU ILICHOMWA MOTO NIKIWA NIMELALA NDANI

Na ASHA BANI, ALIYEKUWA LOLIONDO


AGOSTI 13 mwaka huu, ni siku ya kukumbukwa na baadhi ya familia za wakazi wa Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Siku ambayo wanakijiji wa Ololosokwani Kata ya Ololosokwani mkoani humo walichomewa moto nyumba zao wakapoteza mali ikiwamo mifugo na wanawake kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Tukio hilo la uchomaji wa nyumba linaelezwa kufanywa na Polisi wa Longido, wakishirikiana na wale wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA) ambapo vitongoji zaidi ya 14 viliathirika.

Mmoja wa wanakijiji waliochomewa nyumba zao ni Nasarashi Sereti ambaye anaeleza mkasa mzima na jinsi familia yake ilivyonyang’anywa mifugo.

Nasarashi anasema tukio la kuchomewa moto nyumba zao lilianza Agosti 13 mwaka huu, lakini kwao walivamiwa Agosti 17 kipindi ambacho alikuwa na ujauzito wa miezi tisa.

Anasema akiwa amelala kwa uchovu, watoto wake walipiga kelele za moto katika nyumba yao, akashtuka na kuanza kukimbia kwa bahati mbaya aliangukia sufuria ya maji ya moto iliyokuwa jikoni.

Anasema maji hayo yalimuunguza miguuni na kumuacha akiwa na majeraha makubwa.

Nasarashi anasema alikwenda hospitali kujifungua huku akiwa na majeraha ya moto na uchungu alioupata wakati wa kujifungua.

“Kwa kweli niliteseka mno wakati wa kujifungua, mbaya zaidi nilikuwa nawaza mahali pa kwenda kuishi baada ya kujifungua kwani nyumba yangu ilikuwa imeshateketea,” anasema Nasarashi.

Akiwa mwenye huzuni huku akiwa amemshika mwanawe mchanga, anasema kitendo alichofanyiwa kilimfanya ajione kama si mzaliwa wa nchi hii.

“Tangu wakati huo hadi sasa naishi na majeraha ya moto, huku nikihangaika kumlea mwanangu wa miezi minne kwa shida. Maisha yangu yamekuwa ni ya kutanga tanga kwani sina makazi ya kudumu,” anasema Nasarashi.

Mume wa Nasarashi, Mussa Sereti amabaye ana wake watatu na watoto 15 anasema familia yake yenye jumla ya watu 19 inaishi kwa shida mno kwa kukosa makazi.

Familia hiyo ambayo inalala nje pamoja na mtoto wao mchanga ambaye baridi la usiku humuumiza, inasema imekabidhi maisha yao mikononi mwa Mungu.

Mke mwingine wa Sereti mwenye watoto wanane, anasema wamekuwa na maisha ya kutanga tanga hivyo wanaiomba serikali iwasaidie kwa kuwapatia ulinzi na mifugo mengine itakayowasaidia kujikimu kimaisha.

Naye mke wa tatu, Kijalo Sereti mwenye watoto wanne anaeleza namna wanavyotaabika kwa kukosa makazi maalumu na mifugo iliyokuwa ikiwasaidia kujikwamua kimaisha.

Anasema walikuwa wakitegemea mifugo kuhakikisha watoto wao wanapata maziwa kila siku, lakini sasa wanaishi kwa kula ugali tu kila siku, jambo ambalo hawajalizoea.

Hata hivyo, maisha ya wakazi wa Loliondo yamekuwa shakani kutokana na vitendo mbalimbali vinavyoendelea, licha ya serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kupiga  marufuku vitendo  hivyo vya kinyama.

 

MIFUGO KUPIGWA MNADA

Mifugo zaidi ya 618 ilikamatwa kwa nyakati tofauti katika Hifadhi ya Serengeti na Pori Tengefu la Loliondo.

Mifugo hiyo ilipigwa mnada na Kampuni ya Udalali ya Ubapa, baada ya amri ya Mahakama ya Mugumu iliyopo wilayani Serengeti kutoa agizo hilo kwa kile kilichodaiwa kuwa wenye mali walishindwa kwenda kuwachukua.

Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Tumbesi Saingeni, anasema yeye alinunua ng’ombe 80 kwa gharama ya Sh milioni 7.3 lakini risiti aliyopewa iliandikwa Sh 400,000 jambo ambalo si halali.

Wilson Kilomka mkazi wa Osero Ololosokwani anasema mifugo yake ilinyang’anywa yote na kupigwa mnada na hivyo amebaki hana cha kutegemea.

Naye Ngirimba Tanini anasema alikuwa na ng’ombe 220 wote wamechukuliwa na kuwaacha maskini na kutangatanga na maisha  kwa kuwa tegemeo lake lilikuwa ni mifugo.

Wafugaji hao wanasema huwalazimu kukopa kwa riba ili kununua mifugo mingine.

 

KAULI YA MBUNGE

Mbunge wa jimbo hilo, Willium Tate Olenasha anawahakikishia wakazi wa Loliondo kwamba mgogoro huo utakwisha ndani ya mwezi mmoja.

Katika hatua nyingine, wananchi wa vijiji na kata za Loliondo na Sale,  walikuatana na kutoa tamko la pamoja  kwa kuiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na kitendo hicho akiwamo Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mathew Siloma anasema kitendo hicho kimesababisha madhara makubwa kwa wananchi.

 

MGOGORO

Inasemekana kuwa chanzo cha mgogoro huo ni mamlaka za hifadhi, kutaka kumega eneo la kilometa 1500 katika kijiji hicho na kuliingiza katika Pori Tengefu, jambo ambalo wananchi wanadai hawajashirikishwa na linafanywa kwa kutumia nguvu.

Hadi sasa ng’ombe zaidi ya 628 wameuzwa, 2000 wamekufa na zaidi ya kaya 400 zimeachwa bila makazi.

Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Yannick Ndoinyo anasema mgogoro huo uliodumu kwa miaka 26 sasa umewasababishia umasikini wa kutupwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles