23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Gwajima atoweka

GWAJIMA*Nyumba yake bado yazingirwa, Kamanda Sirro asema hawajui alipo

*Msemaji wa Kanisa ashangaa askari kutimua mbio walipowaona viongozi wa kanisa

 

Veronica Romwald na Asifiwe George, Dar es Salaam

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ametoweka, Jeshi la Polisi limethibitisha.

Kutoweka kwa kiongozi huyo wa kiroho kumekuja ikiwa ni siku moja baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuvamia na kuzingira nyumbani kwake kwa saa kadhaa huko eneo la Salasala, Mtaa wa Kilimahewa, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alikiri kuwa Jeshi hilo linamsaka Askofu huyo kwa mahojiano na kwamba hadi jana lilishindwa kufahamu mahali alipo.

Sirro alisema jeshi lake linamsaka Gwajima likitaka kumuhoji kuhusiana na mahubiri aliyoyatoa kanisani kwake jumapili iliyopita ya Juni 11, mwaka huu.

Wakati Sirro akisema hayo, upo mkanda unaosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikisikika sauti inayofanana na ya Gwajima, ambaye mbali na kujipambanua kumuunga mkono Rais John Magufuli anadai  kuna kiongozi mmoja mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alimfikia na anataka Rais Magufuli asikabidhiwe nafasi ya Uenyekiti wa chama.

Ni mkanda huo ndio ambao unatajwa kuchochea Jeshi la Polisi kumwinda kwa mara nyingine Askofu huyo aliyejizolea umaarufu kwa mahubiri yake ya kuikosoa serikali moja kwa moja na aliyejibatiza jina la Mr. Tanzania.

Jana MTANZANIA Jumamosi lilifika nyumbani kwa Askofu Gwajima na kuweka kambi  katika eneo hilo kwa takribani saa nne lengo likiwa kutaka kuonana naye na kufanya naye mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

Waandishi wa gazeti hili walipofika katika makazi yake 4:45 asubuhi  walishuhudia wanaume watatu wakizunguka zunguka nje ya uzio wa nyumba yake.

Wanaume hao mikononwalikuwa wameshika baadhi ya magazeti yaliyoandika taarifa kuhusu  askari kuizunguka nyumba hiyo jana.

Mwandishi aliwafuata eneo walilokuwa wamekaa na mara na kuwaeleza nia yake ya kutaka kuonana na Askofu hata hivyo walisema wao si wenyeji katika eneo hilo.

“Unafikiri sisi wenyeji… hapana, sisi tunashida na nyumba ile (akionesha kwa kidole), hapa tumekaa tu kwa sababu kule tunaona kuna jua kali, tupo kama wahalifu vile, unaweza kugonga hapo getini lakini sidhani kama unaweza kumpata maana hebu angalia gazeti hili walivyoandika taarifa yao (akimuonesha mwandishi).

“Hivi ndugu yangu unaweza kufikiri na kutueleza pengine unadhani kwanini wanamtafuta namna hii Askofu huyu,” alihoji mmoja wa wanaume hao ambao hata hivyo hawakujitambulisha majina yao.

Hata baada ya mwandishi wa gazeti hili kumjibu kuwa hawezi kujua na kwamba yeye ana shida binafsi na kiongozi huyo wa kiroho mwanaume huyo alimshauri mwandishi kufanya hivyo na kusema haamini kama anaweza kumpata kwa sababu huenda hayupo kabisa katika eneo hilo.

Mwandishi  alikwenda moja kwa moja kupiga hodi katika geti la kuingilia ndani ya nyumba hiyo na baada ya dakika kadhaa alifika mwanamme mmoja ambaye alisema ndani ya nyumba hiyo wamebaki walinzi tu.

“Karibu,… sasa kama ni hivyo si ungeenda kuonana na wale waliokuja jana (juzi), humu ndani tupo walinzi peke yetu, Askofu hayupo kabisa hapa lakini ikiwa unahitaji kauli ya kanisa nenda kaonane na viongozi kule Ubungo kanisani,” alisema.

Hali hiyo ilililazimu gazeti hili kwenda makao makuu ya kanisa hilo, Ubungo ambako mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema viongozi wa kanisa hilo walikuwa katika kikao kujadili suala hilo.

Hayupo Dar

Alipotafutwa msemaji wa kanisa hilo, Yekonia Bihagaze alisema walishangazwa na kitendo cha kuzingirwa kwa nyumba ya Askofu wao huyo licha ya kwamba yupo nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo Bihagaze alisita kuweka wazi mkoa alipo huku akisisitiza kuwa Askofu wao huyo anaendelea na huduma ya neno la Mungu.

“Yupo nje ya Dar es Salaam, anaendelea na mikutano ya injili. Kwa kweli tulishangazwa, tulipoona picha zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikabidi baadhi ya viongozi waende jambo la ajabu walipofika watu wale walikimbia kusikojulikana,”

“Hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa walikuwa askari kwa sababu tunashangaa kwanini walikimbia, unajua tena dunia ya sasa pengine walikuwa majambazi” alisema.

Alisema watu hao walipofika waligonga geti na kufunguliwa na mmoja wa walinzi waliokuwepo wakati huo ambaye walimuweka chini ya ulinzi.

“Mlinzi alitoka kuwafungulia, wakamuweka chini ya ulinzi, swali kubwa walilohoji wapi alipo Askofu kwa sababu ndiye hasa waliyekuwa wakimtaka,” alisema.

Bihagaze alisema kwa kuwa walikimbia baada ya viongozi wa kanisa hilo kufika katika eneo hilo, walilazimika kuwasiliana na Mwanasheria wao Peter Kibatala ili kupata ushauri.

“Kibatala alituambia kama kweli ni askari basi wanaweza kumpata Askofu kwa njia za kawaida kwa sababu viongozi tupo, mwanasheria yupo lakini si kwenda kuvamia nyumbani kwake kama mhalifu fulani.

“Lakini kwa sababu ndiyo hali ilivyo, tunamsubiri mwenyewe arudi baada ya kumaliza mikutano yake kisha atalishughulikia suala hilo,” alisema.

Kuhusu mahubiri

MTANZANIA Jumamosi lilipomuuliza  Msemaji huyo kama mahubiri ya Askofu Gwajima aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu yamesababisha hali hiyo alisema; “Hata mahubiri yenyewe yanayoelezwa hatujui ni ya namna gani kwa sababu mtu anaweza kuhubiri vizuri lakini kwa dunia ya sasa mtu anaweza akaichukua sauti moja akaunganisha na nyingine na nyingine tena ikawa kitu kingine ilihali wewe uliongea jambo zuri.

Mwenyekiti wa Mtaa

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Richard Njela alisema hakuwa na taarifa yoyote juu ya kufika kwa askari hao.

“Upo utaratibu kwa mujibu wa ofisi yetu kuwa askari anapotaka kwenda kwa mtu anakuja na kuandikisha kwenye kitabu nia yake hiyo lakini hawa sikuwaona.

“Sina uhakika kama wale walikuwa askari kweli, taarifa hizo nilizisikia juu juu na baadae mke wangu alinipigia simu na kunijulisha kuwa zimesambaa mtandaoni. Sielewi kwanini walikwenda bila kunijulisha,  kwa sababu wakati ule wa sakata la Askofu Pengo walikuja na nikawapeleka.

Mtendaji  

Naye Jacob Mrema ambaye ni mtendaji wa Kata hiyo alisema ingawa polisi wanaweza kuwa na njia zao za kumkamata mtu wanayemtafuta hata hivyo ingekuwa vyema kama wangewajulisha.

“Sisi tupo karibu na wananchi hata kama wana arresting technique lakini inafaa pia wakitujulisha maana hata hatujui kama walikuwa polisi kweli au wahalifu,” alisema.

Mahubiri yamponza

Akizungumza na MTANZANIA juu ya sakata hilo, Kamanda Sirro alikiri kuwa Jeshi hilo linamsaka Askofu huyo kwa mahojiano.

Alisema linataka kumhoji kuhusu mahubiri aliyoyatoa kanisani kwake jumapili iliyopita ya Juni 11, mwaka huu.

Kuhusu watu waliozingira nyumba ya Askofu huyo, Kamanda Sirro alisema walikuwa ni askari wa Jeshi hilo ambao aliwatuma kwa ajili ya kwenda kufanya upelelezi.

Asakwa kila kona

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher  Fuime alithibitisha kutafutwa  kwa  Mchungaji Gwajima  kwa ajili ya kuhojiwa.

“Askari wetu bado wanaendelea kufanya upelelezi hivi sasa ili kubaini  mahali alipo Askofu huyo kwasababu ametoweka na hata nyumbani kwake hayupo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles