27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli apasua vichwa wasomi

Magufuli+PHOTO*Watofautiana kuhusu staili yake ya uongozi

NA JONAS MUSHI

WANAZUONI wametofautiana kuhusu mwenendo wa uongozi na hatua za kinidhamu zinazochukuliwa na Rais John Magufuli.

Kutofautiana huko kulionekana wazi jana katika mjadala kwenye Tamasha la Kavazi la Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika ukumbi wa jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Katika mjadala huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kavazi la Mwalimu, Profesa Issa Shivji, wanazuoni waligawanyika makundi mawili, moja likiunga mkono mwenendo wa kiuongozi na utendaji wa Serikali ya Rais Magufuli huku kundi la pili likipinga kwa maelezo kuwa haufuati Katiba na Sheria.

Mada katika mjadala huo ilikuwa ‘Mwalimu Nyerere na ufa wa utawala wa Katiba na Sheria,’ ambapo wanazuoni walijadili kwa kina mwenendo wa kiutawala wa Serikali ya awamu ya kwanza katika kufuata Katiba na Sheria dhidi ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano.

Wanazuoni waliounga mkono mwenendo wa Serikali ya awamu ya tano walijenga hoja kwamba rais ana madaraka makubwa aliyopewa kikatiba hivyo yote yanatekelezwa na kusimamiwa sasa na Rais Magufuli ni kwa sababu ya madaraka makubwa aliyonayo.

Kwa upande wa wakosoaji, wao walijikita katika hoja ya kwamba Serikali ya awamu ya tano inaongozwa kwa maamuzi ya mtu mmoja badala ya kufuata sheria na kwamba mwenendo wa kiuongozi wa Rais Magufuli hauna utaratibu unaoeleweka.

Akichangia mada hiyo, Profesa Daudi Mukangara ambaye ni Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema uongozi wa sasa unafanya baadhi ya mambo bila kufuata Sheria na Katiba jambo alilosema kuwa linapaswa kukemewa.

“Hatujui nani atakuja kutawala siku moja na tukiacha mambo haya yaende kama yanavyokwenda ipo siku atatawala mtu ambaye atajiamulia kufanya jambo ambalo halina masilahi kwa umma.

“Mfano kuna suala la matumizi ya fedha, inajulikana kabisa kwa mujibu wa sheria, fedha zote za Serikali zinazobaki kwenye matumuzi ya taasisi za Serikali lazima zirudishwe hazina na zitapangiwa matumizi na Bunge. Labda kama kuna dharura na iwe ya kweli. Lakini si uamuzi wa mtu mmoja kama inavyofanyika sasa,” alisema Prof. Mukangara.

Prof. Shivji katika mchango wake kwenye mada hiyo, alisema utawala usiofuata Sheria na Katiba ni utawala holela na una tabia ya kuwafanya watu wawe na hofu kwa sababu wanakuwa hawajui lini na nini kitawatokea wakiwa kazini.

“Tatizo la utawala holela ni kwamba, unaleta hofu katika jamii na siku zote jamii yenye hofu ndiyo mwanzo wa kutotawalika. Lazima viongozi wafuate misingi ya kikatiba na kisheria, haijalishi Katiba hiyo ni nzuri au mbovu,” alisema Shivji.

Alisema kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, watu ndio wanaotawala lakini wanaongozwa na Sheria na Katiba katika kuongoza kwao badala ya kutumia utashi wao.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikikiuka haki za binadamu ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba ikiwemo haki ya kupata habari na kujieleza.

Hata hivyo, alisema iwapo raia watajua haki zao hawatakuwa na sababu ya kuwa na hofu.

“Wapo watu wanaoogopa hadi wanaogopesha na wengine. Kama mtu unaogopa ogopa kivyako lakini kama unajua haki zako huwezi kuogopa,” alisema Dk. Bisimba.

Wakati wanazuoni hao wakikosoa mwenendo wa kiutawala wa Serikali ya Rais Magufuli, kundi jingine la wanazuoni waliohudhuria mjadala huo liliuunga mkono akiwemo Profesa Josephat Kanyanywi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alisema rais hawezi kulaumiwa kwa hatua anazochukua sasa kwa sababu utawala wake unatokana na madaraka makubwa aliyopewa na Katiba.

“Viongozi wetu wa zamani wamewahi kusema kuwa endapo wangetaka kutawala kidikteta wangeweza kutokana na kupewa mamlaka makubwa katika Katiba. Rais hana vigezo, taratibu wala kanuni zinazomwongoza, amepewa mamlaka makubwa kama mfalme wa kufanya mambo mengi anavyotaka.

“Kwa sasa hivi rais anatumia busara zake na hivyo tukiwa na rais ambaye hana busara atatumia mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Katiba kufanya mambo anavyotaka,” alisema Prof. Kanyanywi.

Mwingine aliyetetea mwenendo wa kiuongozi wa Serikali ya Rais Magufuli ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Mkwawa, Profesa Bernadeta Kilian ambaye alisema mambo anayoyafanya Rais Magufuli yanatokana na mazingira yaliyopo ya kukithiri kwa rushwa na ufisadi.

“Kila awamu imekuwa ikija na mambo yake, awamu iliyopita tuliona uhuru wa kutosha wa watu kusema na hata kwa waandishi wa habari. Lakini ndio uongozi uliokuwa na mambo ya rushwa na ufisadi,” alisema Prof. Kilian.

Mwanazuoni huyo alisema bado ni mapema kuanza kuupima uongozi wa Rais Magufuli kwa sababu uko madarakani kwa kipindi kifupi ambacho hakiwezi kufanyiwa utafiti.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles