Patricia Kimelemeta – Dar es Salaam
ZAIDI ya asilimia 75 ya wanaume wamewakataa watoto wao, hali inayosabababisha ongezeko la watoto wa mitaani jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa na Mkaguzi wa Polisi Dawati la Jinsia la Kituo cha Polisi Oysterbay, Prisca Komba katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya mkakati wa ‘tunaweza kupinga vitendo vya ukatili’ uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema taarifa zilizotolewa kwenye dawati hilo zinaonesha wanaume hao wamekuwa na tabia ya kuwapa mimba wanawake na kuwakimbia ili kwenda kuwapa tena mimba wanawake wengine bila kuwasaidia kulea mimba hizo au mtoto.
“Zaidi ya asilimia 75 ya kesi zilizofika kwenye dawati letu zimesababishwa na wanaume kukataa watoto wao, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
“Hivyo Jeshi la Polisi litashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanatoa elimu ya kujitambua ili kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo zimechangia kuongezeka kwa watoto wasiokua na matunzo bora ya wazazi wao.
“Kuna kila sababu ya kuanzisha mkakati wa kitaifa ambao utashirikisha wanaume na wanawake kwa ajili ya kutoa elimu juu ya madhara yatokanayo na kuwakataa watoto, jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo,” alisema.
Alisema, licha ya kujitokeza kwa tatizo hilo, lakini pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wazazi hao huku jamii ikifumbua macho.
Prisca alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa vitendo vya rushwa ili kuficha ukweli kwenye taarifa za ukatili zinazowasilishwa kwenye mamlaka husika ikiwamo polisi au mahakamani.
“Jamii imekuwa ikishindwa kutoa ushirikiano kwenye taarifa za matukio ya ukatili yanayotokea kwenye jamii yao, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa vitendo hivyo,”alisema.
Hata hivyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Grace Mbwillo, alisema Serikali inatarajia kuzindua mpango maalumu wa kufuatilia vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini.
Alisema, mpango huo utashirikisha wadau mbalimbali ili kupata taarifa za vitendo hivyo ili wahusika watakaobainika kufanya ukatili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Serikali haitawavumilia watu wanaoendelea kufanya ukatili nchini, hivyo basi tutazindua mpango maalumu ambao utashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu vitendo vinazofanywa na baadhi ya watu ili waweze kuchukuliwa hatua,”alisema Mbwillo.