Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAKATI wiki ya Azaki ikitarajiwa kuanza kesho jijini Dodoma ,Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Christian Blind Mission (CBM),Nesia Mahenge amesema asasi za kiraia zipo katika mchakato wa kufanya utafiti wa kujua ni mchango gani wameutoa katika shughuli mbalimbali.
Amesema utafiti huo utasaidia kutoa picha kamili kuweza kuonesha mchango ambao asasi za kiraia wanautoa kwa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 22,2021,mkurugenzi huyo amesema kuna mambo mengi ambayo asasi za kiraia zimefanya kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijijini ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu na kutoa huduma mbalimbali.
Amesema wamekuwa wakifanya shughuli za kuleta maendeleo kwa kushirkiana na Serikali na wamepewa miongozo katika kuingia ubia wa kuleta maendeleo.
Amesema wanafanya shughuli katika sekta za elimu,kilimo,afya na masuala ya ajira, kuwajengea uwezo na maeneo mengine.
“Na kuna tafiti tunataka kuufanya na tumeishaanza mchakato kuweza kuangalia kwa takwimu maalum ni michango ya kiasi gani kama ni rasilimali fedha,watu,vifaa mbalimbali ambavyo vinatolewa na huduma ambazo zinatolewa kuweza kujua tumefanya kwa kiasi gani.
“Nadhani huo utafiti utasaidia sana kutoa picha kamili kuweza kuonesha mchango ambao tunatoa Tanzania,”amesema
Katika hatua nyingine,Mkurugenzi huyo amesema Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kesho anatarajia kufungua wiki ya Asasi za Kiraia(AZAKI) Mkoani Dodoma ambapo jumla ya Asasi zaidi ya 150 zitashiriki katika maonyesho lengo likiwa ni kuonyesha mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Amesema,pamoja na mambo mengine wiki hiyo inawaleta wadau mbalimbali wa Maendeleo nchini ikiwemo wananchi,Serikali,AZAKI na sekta binafsi ambao wote kwa pamoja watajadili na kusherehekea mchango wa AZAKI katika kuleta maendeleo nchini.
“Tunawaita wadau mbalimbali wa maendeleo kujumuika nasi kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo ushauri wa kisheria,kufahamu kazi tunazofanya na kusherehekea kwa pamoja ,”amesema.
Amesema uzinduzi huo wa wiki ya AZAKI utahudhiriwa na wahisani wa maendeleo wakiwemo ubalozi wa Denmark Utakaowakilishwa na Sascha Mulla na Ubalozi wa Canada útawakikishwa na Ms.Helen Fytche.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa United Nations Association (UNA) Reynald Maeda amewataja viongozi na wageni kutoka Serikalini watakaoshiriki katika uzinduzi huo ni pmaoja na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri,Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe na mwakili kutoka Wizara ya Afya Vickness Mayao.
“Katika kusherehekea mafanikio ya sekta ya AZAKI na ubia Wetu baina ya wananchi maonyesho yatakayofanyika tarehe 23 hadi 24 Oktoba katika ukumbi wa Jakaya Kikwete na kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali kama Profesa Jay,Sheta,Barnabas,Gnako,na wasanii wa Dodoma,”amesema.
Amesema kuwa wiki ya AZAKI hukutanisha wadau wa maendeleo kujadili masuala ya masingi kuhusu ustawi wa sekta pamoja na maendeleo ya Taifa Kwa ujumla.