24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Amwunguza mwanawe kwa kujoa kitandani

Na Abdallah Amiri, Igunga

MWANAMKE mmoja mkazi wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Kulwa Shasumuni, amemwunguza mkono wa kushoto mtoto wake Hassani Faustino (9),  kwa kile alichodai ameshindwa kuanika shuka zake alizokojolea kitandani.

Taarifa za kuunguzwa mkono kwa mtoto huyo zilitolewa na majirani, ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wao.

“Mama huyo amekuwa akimfanyia vitendo vya kikatili mwanae mara nyingi hata tunapomzuia amekuwa akitukaripia na kutuambia hayatuhusu masuala ya mtoto wake,” alisema mmoja wa majirani hao.

Alisema katika tukio la juzi, walisikia sauti ya mtoto Hassan akilalamika huku akisema. “mama nakufa”  ndipo walipochungulia dirishani na kumwona mama huyo akiwa  amemweka mtoto wake kwenye moto wa kuni hali iliyowafanya wapige kelele na hatimaye kumwachia.

Kutokana na tukio hilo mwanamke huyo baada ya kumfanyia ukatili mtoto huyo alimpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, ambapo alilazwa wodi namba 8  huku akiendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya moto.

Akizungumza na mwanadishi wa habari hizi, mtoto Hassan Faustino, akiwa wodini alisema alikojoa kitandani kwa bahati mbaya, lakini mama yake alipogundua kuwa amekojoa alimtaka aanike shuka jambo ambalo alisahau kulifanya.

“Nilikojoa kitandani kwa bahati mbaya na mama aliniambia nianike shuka lakini nilisahau ilipofika mchana aliniita ndani na kuanza kuniadhibu na baada ya muda aliniunguza mkono wa kushoto kwa moto,” alisema mtoto huyo.

Mtoto huyo alisema baada ya kuhisi maumivu makali ya moto alipiga kelele ndipo alipomwachia ingawa alikuwa amepoteza fahamu.

Kutokana na tukio hilo, mwandishi wa habari hizi, alimtafuta mama mzazi wa mtoto huyo, Kulwa Shasumuni,  ambaye alikiri kufanya kitendo hicho.

“Ni kweli nilimwunguza mtoto wangu na sikutarajia kuwa hali ingeweza kuwa hivi ila ni hasira tu zilipanda, awali nilimwambia achukue majivu lakini kumbe yalikuwa na moto,” alisema mama huyo.

Akizungumzia hali ya mtoto huyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Igunga,  Abdallah Ombeni, alithibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa na jeraha la moto katika mkono wake wa kushoto.

Hata hivyo alisema pamoja na kuendelea na matibabu bado hali ya mtoto huyo si nzuri.

Kutokana na ukatili huo, Diwani wa Kata ya Igunga, Charles Bomani (CCM),  amelaani kitendo hicho na kuuomba uongozi wa Serikali ya Wilaya kufanya juhudi za kuokoa maisha ya mtoto huyo ambaye bado amelazwa hospitalini hapo.

Boman, alisema anashangazwa na hatua ya Jeshi la Polisi kushindwa kumchukulia hatua za kisheria mwanamke huyo hadi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles