29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ajenda ya jinsia sasa kumhusisha CAG

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake Jinsia na Makundi Maalumu, imeanza kuandaa miongozo ya ushirikiano na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG), ili kuhakikisha ajenda ya jinsia inatekelezwa katika sekta zote.

Hayo yamebainishwa jana Novemba 17, 2023, jijini Dar es Salaam na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Dorothy Gwajima wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa mawaziri wa fedha na jinsia Afrika wenye lengo la kujadili kuhusu uwekezaji kwa maendeleo ya usawa wa jinsia ambapo jumla ya nchi 22 zimeshiriki.

Amesema katika mkutano huo wametoka na maazimio matano, yote yakiwa na lengo la kusukuma mbele ajenda ya jinsia na kuwa na usawa wa kisera kwa nchi zote za Afrika.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

“Lazima kuwa na jicho la ufuatiliaji ili kujua fedha zilizopagwa je zimetumika katika kuendeleza ajenda au laa? Kwani lengo ni kuendeleza ajenda na kuhakikisha kuna maendeleo yenye usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake,” amesema Dk. Dorothy.

Akisoma maazimio ya mkutano huo amesema mojawapo ni kutizama suala la ukatili wa jinsia ili liweze kuwekewa bajeti kwa ajili ya kupambana nalo.

Amesema pia wamedhamiria kuboresha teknolojia na ubunifu kuelekea usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake lakini pia kumuwezesha na kumpa elimu mwanamke.

Ameongeza kuwa amani imeendelea kuwepo katika nchi kwa sababu wanawake wameshiriki kuhakisha utulivu unapatikana.

Dk. Gwajima amesema mwanamke anapaswa kuwa na kasi kama mwanaume kwenye maendeleo ili wote wawe na mchango sawa kwa nchi.

Aidha amesema wanawake wamekuwa wakifanya shughuli nyingi za kimaendeleo lakini hazijarahisishwa wala kupewa zana za kisasa za kufanyia shughuli zao majumbani.

“Kwa Tanzania wanawake wengi ndio wapo katika kilimo na wanazalisha kweli kweli, kazi yao ni asilimia 80 lakini hawana nyenzo za kufanyia kazi zao lakini bado kuna ukatili wa kijinsia unaowaandama na kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi,”amesema.

Naye Mkurungenzi wa UN Women Kanda ya Afrika Mashariki, Dk.Maxime Houinato, amesema mgawanyo wa haki za wanawake ni chachu ya kukuza uzalishaji na maendeleo katika mataifa.

“Katika kufikia malengo suala la jinsia linahitajika kuwekewa mkazo katika sera na bajeti ili uchumi wa mwanamke uweze kukua kwani uchumi wa mwanamke ukikua na mataifa nayo yanakua,”amesema Dk. Houinato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles