28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

IHI yataka kuongezwa idadi wanaohudumia watoto njiti

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mkurugenzi wa Ifakara Health Institute (IHI), Dk.Honorati Masanja, ametoa rai kwa Serikali kuongeza idadi ya watumishi wa afya idara ya mama na mtoto ili kukabiliana na vifo vya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu(njiti) na kufikia malengo yaliyoweka.

Wito huo ameutoa jana Novemba 17, 2023, jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa pili wa kisayansi kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto na ikiwa ni maadhimisho ya siku ya mtoto aliezaliwa na uzito pungufu (njiti) duniani.

Amesema watumishi wa afya wanatakiwa kuongezeka ili kufikia malengo yaliyowekwa ifikapo mwaka 2030, kuwa na vifo 12 kwa kila vizazi hai 100,000.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dk.Jakaya Kikwete alipotembelea banda la Ifakara Health Institute (IHI) lililopo kwenye Mkutano wa pili kisayansi kuhusu afya ya uzazi mama na mtoto akipata maelekezo jinsi taasisi hiyo inavyofanya kazi.

“Watumishi wa afya idara ya mama na mtoto wanatakiwa kuongezwa ili waweze kutoa huduma stahiki waliokuwepo ni wachache hawatoshi, “amesema Dk. Masanja

Amesema chumba kinacholaza watoto 50 mpaka 70 kinahitaji manesi wengi tena wenye mafunzo ya kuhudumia watoto wachanga na wanatakiwa wapatikane kwa saa 24.

Amesema mpango wa kuongeza watumishi umetokana na mapendekezo ya utafiti wa kisayansi na utaongeza chachu ya kufikia malengo yaliyowekwa.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto Wachanga na Vijana kutoka Wizara ya Afya, Dk. Felix Bundala amesema kwa mwaka watoto elfu 50 wanakufa kati ya vizazi hai 2,200,000 ambapo asilimia 80 ni wenye uzito pungufu.

Amesema kufuatia agizo la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan la kutaka kuanzishwa chumba maalum kwa ajili ya kuhudumia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu kutasaidia kupunguza vifo 30,000 kwa mwaka.

Kwa upande wake daktari wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Nahya Salim amesema Tanzania ina mpango mkakati wa kushusha vifo vya watoto wachanga angalau mpaka 17 kwa vizazi hai 100,000 hadi kufikia 2025.

“Kutokana na ripoti iliyotolewa na wizara ya Afya ya kushusha vifo vya watoto bado kasi ni ndogo sana. Kwa kipindi cha miaka mitano,” amesema Dk. Nahya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles