Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
WASANII wa Bongo Fleva, Whozu, Billnass na Mbosso, wametakiwa kulipa faini ili kuruhusiwa kufanya kazi za sanaa nchini kwa kufuata maadili ya Kitanzania.
Uamuzi huo umefikiwa leo Novemba 14,2023 katika kikao cha kusikiliza rufaa ya wasanii hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Awali Whozu alipewa adhabu ya kufungiwa miezi sita kutojihusisha na sanaa na kulipa faini sh. 3 milioni, huku Bilnass na Mboso miezi mitatu kila mmoja.
Baada ya kikao hicho na adhabu ya kufungiwa kuondolewa, Whozu anatakiwa kulipa faini ya sh. 5 milioni, Mboso sh. 3 milioni na Billnass milioni moja kabla ya kuendelea na kazi zao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro na Naibu wake Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA, msanii Whozu amepewa saa sita ili kutekeleza azimio la kushusha wimbo  wake wa Ameyatimba kwenye “digital platforms” zote kama makubaliano yanavyoelekeza.
Aidha Waziri Ndumaro amewaasa wasanii hao na wengine nchini kutumia ubunifu kwa kufuata taratibu ulioainishwa katika mwongozo wa uzingatiaji maadili katika kazi za sanaa.