Na Ramadhan Libenanga -Morogoro
MBUNGE wa Morogoro Mjini, Aziz Abood (CCM), amesema katika kipindi chake cha ubunge anataka kuweka historia ya kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa asilimia 90.
Abood amesema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi zake kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya chama chake ya mwaka 2015/20.
Alisema kero kubwa ya maji katika Jimbo la Morogoro Mjini inatokana na kasi ya ongezeko la watu katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro.
“Ukuaji wa mji na ongezeko la watu unapelekea kuwepo kwa uhaba wa maji,” alisema Abood.
Akizungumzia mikakati yake mbunge huyo alisema amejipanga kikamilifu kwa kutoa kipaumbele utekelezaji wa ahadi zake katika sekta ya maji.
Alisema kuwa awali Manispaa ya Morogoro ilikuwa na kata 19 lakini kwa sasa kuna kata 29 hali inayochangiwa na kukua kwa mji na ongezeko la watu.
Alisema wakati wote amekuwa akishirikiana na Serikali pamoja na juhudi zake binafsi kama mwakilishi wa wananchi ili kuondoa changamoto hiyo.
Kutokana na hali hiyo aliwaomba wananchi wa Morogoro Mjini wawe na subira wakati utekelezaji wa miradi ya maji ikiendelea katika kata mbalimbali ndani ya manispaa hiyo.
"Tuombe uzima tu na wananchi wangu ili niweke historia Jimbo la Morogoro katika huduma ya maji. Na kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani tunaendelea na mkakati wa kuifanya Morogoro inakuwa jiji hasa kwa kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii,” alisema.