27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

PROF. MAGHEMBE AKUNWA MAFANIKIO KAGERA

Na Mwandishi Wetu, Kagera


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa mkoa huo, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu, kwa kufanikisha operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi.
Pamoja na pongezi hizo, amewaonya watumishi wa hifadhi hizo kupoteza ajira zao endapo wataruhusu mifugo  kurudi tena ndani ya hifadhi hizo.


Alitoa pongezi na tahadhari hiyo jana mjini Bukoba wakati akizungumza na uongozi wa mkoa huo na kusema kazi hiyo ni ya kupongezwa kwakuwa imeleta matumaini ya uhifadhi.


“Nawashukuru kipekee kabisa kwa jinsi ambavyo mlifanya ile operesheni ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi zetu, tulifanya kwa uweledi uliotukuka, hata kama umesikia watu wanalalamika hakuna aliyesema kuku wangu waliuawa, walipigwa risasi, tulinyang’anywa mifugo, kazi hii ilifanywa vizuri na kwa weledi mkubwa sana.


 “Hatutaruhusu tena mifugo irudi ndani ya hifadhi, hili ni jambo kubwa ambalo ni wajibu wa wahifadhi wote kuhakikisha  kwamba hakuna mifugo itakayokuwa inaingia humo ndani. Kuanzia sasa kama tutakuta mtu ameingia kwenye hifadhi yako wakati tunamwondoa, tunamwondoa yeye na wewe na familia yako yote ili mbegu yako mbaya isibaki katika uhifadhi wa wanyamapori,” alisema.


Alisema ili kuimarisha ulinzi katika hifadhi hizo, utaratibu wa kutumia ndege maalumu za doria na “drones” (ndege zisizo na rubani), utawekwa ili kuwabaini wahalifu watakaokuwa wamekaidi agizo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.  


“Tutakuwa tunarusha ndege mara moja kila baada ya wiki tatu au wiki mbili kuhakikisha kwamba, hakuna mtu anaingia na mifugo humo ndani lakini pili tutafanya doria na ndege zile ambazo hazina marobani kuhakikisha kwamba tunaangalia kinachotokea humo ndani wakati wote.

“Najua wanaweza kubadilisha “system” (utaratibu), ikawa ya usiku na hawa askari hawa tutawapa mafunzo maalumu chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuanzia miezi sita mpaka tisa, wajifunze namna ya kuhangaika na hawa ambao wanaingia kwenye hifadhi zetu,” alisema. 


Akizungumzia operesheni hiyo, alisema ulitolewa muda maalumu kwa watu kutoa mifugo yao kwa hiari katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu mkoani humo ambapo wale wote waliotii hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yao ispokuwa wale waliokaidi walifikishwa mahakamani na mifugo yao ikataifishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kifungu namba 111 sehemu ya kwanza ambayo inaruhusu kutaifisha mali itakayokutwa hifadhini.


Naye Meja Jenerali Mstaafu Kijuu, alishukuru  ushirikiano alioupata kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi chote cha utekelezaji wa operesheni hiyo.
Alisema wamepata mafanikio makubwa ikiwamo wanyamapori kuanza kurudi kwenye maeneo yao katika mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi.


Operesheni ya kuondoa mifugo na wananchi waliovamia Hifadhi ya Misitu ya Biharamulo, Nyantaka na Ruiga na mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi mkoani Kagera, ilianza Machi 30, 2017, jumla ya mifugo 5,939 ilikamatwa, ikiwamo ng’ombe 5,754, mbuzi 140, kondoo 45 na watuhumiwa 185 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles