SABABU KIFO CHA MBUNIFU NEMBO YA TAIFA YATAJWA

0
566

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM


MBUNIFU wa nembo ya Taifa (bibi na bwana), Francis Maige maarufu Ngosha, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema Ngosha alifariki juzi saa nne usiku wakati madaktari wakiendelea kumpatia matibabu.

Alisema awali alikuwa akiendelea vizuri na matibabu kabla hali yake kubadilika ghafla siku hiyo na kufariki dunia.

“Juzi Rais John Magufuli alikuja kumtembelea, hali yake ilibadilika ghafla na kuwa mbaya, jioni ile hakuweza kula wala kuongea, ilibidi madaktari wamsaidie. Lakini ilipofika usiku alifariki dunia,” alisema.

Profesa Museru alisema madaktari walikuwa bado wanamfanyia uchunguzi Ngosha iwapo alikuwa akisumbuliwa na kifua kikuu au maradhi mengine.

 “Kwa sababu alikuwa na matatizo, alipata ‘infection’ kwenye kifua na tayari walikuwa wamemwanzishia matibabu ya dawa na hata hivyo afya yake ilikuwa bado haijawa nzuri sana,” alisema.

Ngosha alifikishwa hospitalini hapo hivi karibuni akitokea Hospitali ya Amana ambako uchunguzi wa awali aliofanyiwa hospitalini hapo ulionyesha alikuwa anakabiliwa na tatizo la utapiamlo.

Mzee huyo ambaye alisema amezaliwa mwaka 1931, hakubahatika kupata watoto na marehemu mkewe.

“Nilikuwa naishi na mke wangu tangu mwaka 1977, tulipanga huko Buguruni, lakini yeye amefariki kwa ajali ya gari, hatukujaliwa kupata watoto, wale walionipangisha wananifadhili, hivi sasa silipi kodi ya chumba,” alisema.

Alisema yeye ni mwenyeji wa Misungwi, Kijiji cha Bulima, ambako alisoma katika Shule ya Msingi Misungwi darasa la kwanza hadi la nne na kisha kuhamia katika Shule ya Msingi Bwiru ambako alimalizia elimu yake ya msingi.

“Nina dada zangu ambao wamejaliwa watoto, wako huko Sengerema, lakini bahati mbaya simu yangu iliharibika, hivyo sina mawasiliano nao kwa muda mrefu na hawajui kama ninaugua hivi sasa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here