LEONARD MANG’OHA NA RAHMA SWAI (TSJ)
SHIRIKA la ndege la Fastjet Tanzania limeanza kuwarejeshea nauli wateja walionunua tiketi baada ya kusitisha safari zake.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Desemba 17, mwaka huu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuliagiza shirika hilo kuwarudishia fedha abiria wote walio kata tiketi au kuwatafutia nafasi za safari katika mashirika mengine.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Msemaji wa shirika hilo, Lucy Mbogoro, alisema baadhi ya wateja wao walianza kurudishiwa fedha hizo Jumatatu wiki hii hasa kwa wateja walionunua tiketi kwa njia ya mtandao.
Kuhusu wateja waliolipia tiketi kwa fedha taslimu, alisema wanaendelea na mchakato wa kuwarudishia na alidai zingeanza kurejeshwa jana kuanzia saa 9 alasiri.
“Jumatatu tulitoa tangazo kuwa tutaanza kushughulikia malipo ya wateja wetu pamoja na wadau wengine tunaofanya nao biashara, siku hiyo hiyo tulianza kushughulikia kwa wale walionunua kwa M-Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa.
“Ila kwa wale walionunua kwa ‘cash’ tulitangaza tutaanza kushughulikia malipo yao tarehe 20 na tayari tumeanza kulishughulikia hilo leo (jana) saa 3:00 asubuhi, tumekuwa tukiendelea na taratibu za benki kwa sababu hatuwezi kukaa na fedha nyingi, lazima tuzipeleke benki, muda mfupi ujao wataanza kurejeshewa fedha zao,” alisema Lucy.
Alisema katika urejeshaji wa fedha hizo, watatoa kipaumbele kwa wateja waliotarajia kusafiri kuanzia Desemba 20, hadi 31, mwaka huu ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao, huku wale wanaotarajiwa kusafiri kuanzia Januari, wakiendelea kulipwa taratibu.
“Kumbuka TCAA hawakusema Fasjet imefungiwa kwa hiyo tutendelea na malipo na kila mmoja atapata haki yake, lakini wako baadhi ambao hawahitaji kurejeshewa fedha na wamesema kama shirika litaanza kurusha ndege hivi karibuni wataendelea kusubiri,” alisema Lucy.
MTANZANIA lilishuhudia abiria wengi waliofika katika ofisi za shirika hilo zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam.
Mmoja wa abiria hao, Juma Jeremiah ambaye alikata tiketi ya kuondoka Januari 5, mwakani alilalamikia utaratibu uliotumika kuwarejeshea fedha zao na kudai huenda hawana fedha.
“Hapa leo (jana), tumekuja wamechukua maelezo na kuhakiki tiketi, naona bado hawajajipanga… hii ni ndege si basi, taarifa za wateja zote ziko kwenye mfumo, kwahiyo hakukuwa na sababu ya kutuita hapa,” alisema Jeremiah.
Abiria mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alidai alikumbwa na adha ya usafiri Desemba 14, mwaka huu jijini Mwanza baada ya kukosa ndege na kulazimika kusafiri kwa basi kwenda Dar es Salaam.
Desemba 17, mwaka huu, TCAA ililiandikia notisi ya siku 28 shirika hilo na kulitaka kujieleza kwanini lisifutiwe leseni ya kuendesha biashara hiyo nchini baada ya kukosa sifa, ikiwamo kutokuwa na ndege baada ya moja kati ya mbili zilizosajiliwa nchini kuharibika na kupelekwa nje ya nchi kwa matengenezo, huku moja ikizuiwa na mamlaka hiyo.
Sababu nyingine, ni shirika hilo kukabiliwa na madeni makubwa kutoka kwa taasisi zinazolidai, ikiwamo TCAA ambayo inadai zaidi ya Sh bilioni 1.413 na kutokuwa na meneja uwajibikaji ambaye ni lazima awe mtaalamu wa masuala ya kiufundi ya ndege.
Ikumbukwe hivi karibuni shirika hilo lilifanya mabadiliko ya umiliki baada ya aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kupitia kwa Ofisa Uhusiano na Masoko wa Fastjet, Lucy, alitangaza kununua asilimia 64 ya hisa za kampuni hiyo, hivyo kuongeza hisa zake kufikia asilimia 68 kutoka nne alizokuwa akimiliki awali.
Ununuzi wa hisa hizo ulitajwa kuwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha shirika hilo kuelekea mikakati mipya ya kuboresha huduma zake.
Inadaiwa Masha ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet, alinunua asilimia 17 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni mama ya Fastjet PLC ya Afrika Kusini na asilimia 47 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na wawekezaji wazawa, ikiwa ni mpango wa kuifanya imilikiwe moja kwa moja na Watanzania.