29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Taasisi ya uongozi kitovu cha misingi ya maadili

Na Ismail Ngayonga

UTAWALA bora ni mfumo wa uongozi unaozingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji, misingi ya haki na sheria kuwa wzesha viongozi na watendaji katika utumishi wa umma kufanya kazi kwa ufanisi na uadilifu kwa manufaa ya jamii.

Mfumo huu ukizingatiwa katika uongozi wa jamii au taifa, unahakikisha kwamba demokrasia ya kweli inafanya kazi yake na vyombo vyote vya mamlaka vinatenda kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa na kuheshimu mipaka ya mihimili ya dola.

Kwa mantiki hiyo ni wazi kwamba nchi yoyote yenye kujenga demokrasia ya kweli, lazima ihakikishe kwamba inajenga misingi imara ya utawala bora na vyombo imara vya mamlaka na si kujenga uongozi unaomtegemea mtu mmoja au kikundi cha watu wachache.

Ili kutekeleza dhana ya utawala bora mambo yafuatayo lazima yazingatiwe, ambayo ni pamoja na matumizi sahihi ya dola, matumizi mazuri ya madaraka, kujua na kutambua madaraka waliyonayo na matumizi yake na madaraka yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na Katiba na Sheria.

Thamani na heshima ya kiongozi kwa anaowaongoza ipo katika uwezo wake katika kupambanua mambo kimkakati, kuwaelewesha na kuwajengea hamasa anaowaongoza ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, anasema Serikali imeendelea kuwasisitiza waajiri wote nchini kuwapeleka watumishi wao Taasisi ya Uongozi ili kuwajengea uwezo katika namna ya kufanya kazi za utumishi wa umma.

Mkuchika anasema Serikali kupitia Taasisi ya Uongozi imeendelea kusimamia malengo yake ya kuwa kituo cha utaalamu wa hali ya juu cha kuendeleza viongozi barani Afrika kwa kuanzia na Tanzania, Ukanda wa Afrika Mashariki na hatimaye Afrika kwa ujumla wakiwamo viongozi waandamizi waliopo na wanaojitokeza wakiwemo wanasiasa, watumishi wa Serikali na Mahakama.

Mkuchika anasema katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, Taasisi ya Uongozi imetoa Mafunzo ya Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (Post Graduate-Diploma in Leadership) iliyozinduliwa  Aprili 21, 2017 ambayo inalenga kuwajengea viongozi uwezo wa kufanya uamuzi wa kimkakati, kusimamia rasilimali watu na rasilimali nyingine na kujenga sifa binafsi za kiongozi.

“Programu hii inatekelezwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto kilichoko Helsinki, Finland, ambapo  hadi kufikia Machi, 2018 moduli nane (8), zimetolewa katika awamu ya kwanza imehusisha maofisa waandamizi 30 wa Jeshi la Polisi huku awamu ya pili ikiwahusisha maofisa waandamizi 30 kutoka wizara, taasisi na mashirika ya umma mbalimbali,” anasema Mkuchika.

Akifafanua zaidi mafunzo hayo, Waziri Mkuchika, anasema Serikali imeendesha kozi nane za muda mfupi kwa viongozi 238 wa umma ili kuimarisha utendaji kazi katika maeneo ya uongozi wa kimkakati, utawala, mitazamo na dira, majadiliano ya mikataba yenye thamani kubwa, kiongozi mwadilifu na uongozi binafsi na wenye maadili.

Kuhusu programu za kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali, Waziri Mkuchika, anasema Serikali iliendesha programu maalumu kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa mamlaka za Serikali za Mitaa iliyolenga katika kuwajengea uwezo katika masuala ya maadili, utawala bora na uwajibikaji, mawasiliano fanisi, utendaji wenye matokeo, uongozi wa kimkakati, usimamizi wa vihatarishi na udhibiti wa ndani, mahusiano kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji.

“Kwa kushirikiana na Taasisi za ndani na nje ya nchi, makongamano matano (5) ya kimataifa, kikanda na kitaifa yalifanyika kwa lengo la kukutanisha viongozi ili kubadilishana taarifa, maarifa na uzoefu na kuwaongezea uelewa wa masuala ya uongozi na maendeleo endelevu, ambapo viongozi 826 walishiriki kutoka Tanzania na nchi za Kenya, Rwanda, Somalia, Afrika Kusini, Botswana, Msumbiji na Malawi.

Anayataja mataifa mengine kuwa ni pamoja na Mali, Ghana, Ethiopia, Jamhuri ya Watu wa Kongo, Nigeria, Sierra Leone, Liberia, Ivory Coast, Namibia, Niger, Togo, Zimbabwe, Trinidad na Tobago, Amerika, Uingereza, Ujerumani, Ubelgiji, Sweden, Canada na Australia.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika, katika masuala ya utafiti, Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza ziliendesha utafiti kuhusu “Viwezeshi na Vikwazo vya Uongozi barani Afrika” na kuhusisha mataifa matano ya Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokarasi ya Kongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles