33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Kabudi ateta na mabalozi wa Africa nchini

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, amekutana na mabalozi wa Afrika wanaowakilisha mataifa yao nchini ambao wamezungumzia mambo mbalimbali ikiwamo Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Akizungumza katika kikao hicho, kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa mabalozi wa Afrika nchini, Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed, alitaka nchi za Afrika kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi jambo litakaloliwezesha bara hilo kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu.

Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya utaratibu wa Serikali kukutana na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.

Kiongozi huyo wa mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, alisema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara hilo linaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara hilo kujitegemea. 

Naye Balozi wa Kenya hapa Nchini, Dany Kazungu, alisema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.

Naye Profesa Kabudi alitumia fursa hiyo kuwaeleza mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za binadamu lakini pia kutumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.

Mkutano huo uliohudhuriwa mabalozi 15 na wawakilishi wa balozi nane ambao walitumia fursa hiyo kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kama baba wa demokrasia Afrika pamoja na kuuombea Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles