26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Simba kuitetemesha Dar

Na WINFRIDA MTOI- DAR ES SALAAM

KILELE cha maadhimisho ya siku ya Klabu ya Simba maarufu Simba day, kimepangwa kuwa leo, ambapo litapigwa pambano la kimataifa la kirafiki kati ya Wekundu hao na miamba ya soka la Burundi, timu ya Vital’o.

Pambano hilo litarindima kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini likitanguliwa na burudani mbalimbali ikiwemo  ya muziki.

Klabu ya Simba imekuwa ikiadhimisha siku yake
kila ikikapo Agosti 8, lakini mwaka huu ililazimika kusogezwa mbele baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuchelewa kufikia tamati kutokana na janga la corona.

Mchezo huo kama ilivyokuwa kwa mingine iliyopita ya siku ya klabu hiyo, utatumika kutambulisha kikosi kitakachotumika msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano mengine.

Lakini kiu ya wapenzi wengi wa Simba ni kuwashuhudia wachezaji wapya waliosajiliwa kipindi hiki cha dirisha la usajili wa msimu ujao.

Timu hiyo imesajili wachezaji saba wapya, kati yao wanne wa kigeni na watatu wazawa.

Wazawa ni mabeki David Kameta(Lipuli), Ibrahim Ame(Coastal Union) na mshambuliaji Charles Ilafya, Timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC).

Kwa upande wa wachezaji wa Kimataifa watakaopamba tamasha hilo ni viungo Bernard Morrison, ambaye ni raia wa Ghana, aliyemaliza mkataba na Yanga, Larry Bwalya(Power Dynamos, Zambia), beki Joash Onyango(Gor Mahia, Kenya) na mshambuliaji Chrispine Mugalu, Lusaka Dynamol,DRC.

Hamu kubwa ya mashabiki hao wa Simba ni kuwaona nyota hao wakiwa uwanjani wamevalia jezi nyekundu, hasa Morrison ambaye amekuwa kivutio kikubwa kutokana na kusajili akitokea kwa watani wao Yanga.

Morrison amekuwa gumzo kubwa kwa Wanasimba na kitu kikubwa wachotarajia kutoka kwake ni  kufanya vile vitu vyake vya kupanda juu ya mpira akiwa anacheza mechi.

Kwa kawaida katika tamasha hilo la Simba Day, licha ya kutaka matokeo mazuri ya mchezo huo, lakini jambo kubwa linalowavuta mashabiki hao ni zile burudani zinazokuwepo uwanjani.

Msanii nyota wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platinum, anatarajia kutumbuiza katika kilele hicho.

Wasanii wengine wanaotarajia kuamsha shengwe ni Mwasiti Almasi, Khalid Ramadhani, maarufu Tundaman na wengine wengi.

Akizungumzia tamasha hilo Diamond alisema “Mashabiki waje kwa wingi kwangu nimepania kufanya shoo ya nguvu, kama mnavyojua ni muda mrefu umepita sijafanya shoo kwahiyo kina arosto(kiu).”

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, alisema tamasha hilo litakuwa la aina yake, huku akiahidi ‘surprise’ kwa mshabiki wao.

Alisema watatumia viwanja viwili, Uwanja wa Taifa na Uhuru ambao wataweka TV kubwa, ili kutoa nafasi kwa mashabiki wengi kushuhudia  shamra shamra hizo.

“Ukiachana na Diamond, kesho(leo) kutakuwa na ‘surprise’, watu waje kwa wingi, wajionee wenyewe,” alisema Mo.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck, alisema kikosi chake kinatarajia kuonyesha mchezo mzuri.

“Mchezo wa kesho (leo) ni wa kufurahisha   mashabiki, ni siku ya kufurahi, wachezaji  tuliokuwa nao msimu uliopita na wapya wote watatambulishwa,”alisema Sven.

Tamasha hilo lilizinduliwa mwanzoni mwa wiki hii,ambapo wapenzi wa klabu hiyo nchi nzima, lakini pia wachezaji wa kikosi cha timu hiyo wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles