27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm: sitobadili kikosi cha Mapinduzi

hans-van-der-pluijm-kocha-wa-yangaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema hatoweza kubadili kikosi chake katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na kushindwa kunyakua Kombe la Mapinduzi.

Yanga ilitolewa katika nusu fainali na timu ya URA Januari 8 mwaka huu, baada ya kupata sare ya 1-1 na kulazimika mchezo huo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti na kujikuta ikifungasha virago kwa kufungwa penalti 4-3.

Timu hiyo ipo nafasi ya pili katika Ligi Kuu kwa kuwa na pointi 33, ambapo inajiandaa kuvaana na timu ya Ndanda ya Mtwara iliyoko nafasi ya 13 ikiwa na pointi 9 baada ya kucheza michezo 13.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Boko Veterani ulioko Dar es Salaam, Pluijm alisema mchezaji yeyote ataweza kupata nafasi ya kucheza kutokana na kiwango chake.

“Kikosi changu kipo vizuri kuanza Ligi Kuu bila ya wasiwasi, lakini sitakurupuka kubadili kikosi eti kwa kuwa kilishindwa kunyakua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi,” alisema Pluijm.

Pluijm alisema kwamba, kwa sasa timu yake inajiandaa kukutana na timu ya Ndanda, huku akiamini kwamba mchezo utakuwa mgumu licha ya wapinzani wake kuwa nafasi ya chini.

“Hatuwezi kudharau timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu, hivyo tunaendelea na mazoezi na kujiweka vizuri kabla hatujavaana na timu hiyo.

“Katika Mapinduzi tulipambana kadiri tulivyoweza lakini bahati haikuwa yetu, akili yetu tunairudisha kwenye michuano ya ligi hivyo tunawataka mashabiki watarajie kiwango bora,” alisema Pluijm.

Akimzungumzia kocha mpya msaidizi wa Simba, Jackson Myanja, alisema kwamba atakuwa na changamoto kubwa kutokana na wachezaji wa timu hiyo kuwa katika hali mbaya kifedha.

“Mayanja anajidanganya tu anakomaa kuwafundisha wachezaji ambao wameathirika na migogoro ya uongozi na kutolipwa fedha zao kwa wakati,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles