22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kaburu acheza kama Pele Zanzibar

Geoffrey-Nyange-KaburuNA MICHAEL MAURUS, ZANZIBAR

MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, amecheza kama Pele baada ya kufanikiwa kuwateka viungo wawili wa URA ya Uganda, Said Kyeyune na Oscar Agaba ambao waliwafunika wenzao wa Yanga, walipocheza nao katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani hapa Jumapili iliyopita.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, URA ilipata ushindi wa penalti 4-3 na kutinga fainali, ikiwa ni baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Yanga ndiyo iliyouanza mchezo huo kwa kumiliki kiungo kupitia viungo wao, Mbuyu Twite na Thaban Kamusoko, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda, Kyeyune, Agaba na Julius Ntambi walionekana kucharuka na kuwazidi ujanja viungo wenzao hao wa Jangwani.

Ni kutokana na umahiri wao, mwisho wa siku Twite alijikuta akiwa hoi na kuomba ‘sub’ na kumwacha Kamusoko na Salum Telela ambao hawakufua dafu kwa Waganda hao.

Baada ya kushuhudia uwezo wa viungo hao, imeelezwa kuwa Kaburu alianza ‘fujo’ zake kwa kuzungumza nao kuona iwapo anaweza kuwatwaa.

Katika kuonyesha jinsi alivyokuwa ‘siriazi’ na viungo hao, kiongozi huyo anayesifika kwa umafia wake linapokuja suala la kumwania mchezaji yeyote yule, juzi alijitokeza kwenye Uwanja wa Amaan kujiridhisha zaidi juu ya uwezo wa wakali hao wakati walipokuwa wakivaana na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo.

Kama walivyokuwa wakitegemewa, viungo hao walifanikiwa ‘kujiuza’ kwa Kaburu baada ya kuonyesha uwezo mkubwa na kuisaidia timu yao kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi mnono wa mabao 3-1.

Akizungumzia juu ya tetesi za kuhusishwa kwake na Simba, Kyeyune alisema kuwa akiwa kama mchezaji anayesaka maisha na mafanikio kupitia soka, yupo tayari kujiunga na Wekundu wa Msimbazi hao.

“Simba ninaifahamu kama timu kubwa hapa Tanzania na Afrika Mashariki, iwapo watanitaka nipo tayari kufanya kazi, kwanza uchezaji wao unanivutia sana, wanacheza soka la pasi sana, hii ndiyo staili yangu, napenda sana kuchezea mpira ili kuwapa burudani mashabiki,” alisema.

Gazeti hili liliwasiliana na Kaburu kufahamu kama kweli wana mpango wa kusajili mchezaji yeyote wa URA au wa timu nyingine yoyote ile ambapo alisema: “Usajili umefungwa, hatuna mpango wa kusajili mchezaji yeyote wa URA, kikosi chetu kipo vizuri na kina wachezaji wazuri ambao tunaona watatutosha.”

Alipobanwa zaidi sababu za kuendelea kuwapo visiwani hapa wakati timu yake ikiwa imeshatolewa kwenye michuano hiyo, alicheka na kusema: “Mimi ni kiongozi wa timu ya mpira, hivyo ninapoona sehemu kunachezwa mpira ni wajibu wangu kuwepo, Simba ni watu wa mpira na si wababaishaji kama ilivyo kwa klabu nyingine… mwenyewe unaona ni kiongozi wa timu gani nyingine yupo hapa uwanjani leo (juzi)?

“Lakini pia iwapo nitamuona mchezaji mzuri, siwezi kumuacha hivi hivi, hakuna kiongozi wa timu ambaye atamuona mchezaji mzuri na kumwachia… hivyo kama kuna mchezaji yeyote atatuvutia, tutazungumza naye.”

Habari zilizozagaa visiwani hapa ni kwamba uwapo wa Kaburu ulilenga kuwafuatilia viungo hao wa URA, pamoja na Shizza Kichuya na Ibrahim Jeba wa Mtibwa Sugar.

Ikumbukwe Simba iliaga michuano hiyo ya Mapinduzi baada ya kutolewa na Mtibwa ilipokubali kipigo cha bao 1-0, shujaa wa Wakata Miwa hao wa Turiani, akiwa ni Jeba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles