Ashura Kazinja, Â Morogoro
AGIZO la Rais John Pombe Magufuli la kuwajengea vibanda wafanyabiashara wa wa eneo la Dumila mkoani Morogoro, walio kandokando ya barabara ya Dodoma-Morogoro, limeanza kutekelezwa.
Hatua hiyo inayotekelezwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, imekuja siku chache tangu Agosti tano ambapo Rais Magufuli aliagiza wafanyabiashara hao kujengewa vibanda vya kufanyia biashara zao.
Ili kutekeleza agizo hilo Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Kalobelo na timu yake juzi walifika katika eneo hilo kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo kwa kufanya tathmini ya jinsi ya kupanua barabara katika eneo hilo ili kujenga vibanda hivyo vya wafanyabiashara.
Akiwa katika eneo hilo la Dumila Kalobelo alisema agizo la Rais limeanza kutekelezwa kuanzia Agosti 6 na ifikapo Agosti 10 vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kazi hiyo vitawasili eneo la tukio na kazi kuanza mara moja.
Aidha Kalobelo alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Asajile Mwambambale, kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuanza ujenzi wake haraka badala ya kusubiri fedha zilizo ahidiwa na Rais.
Vilevile aliwaagiza wataalam wanaochora michoro ya vibanda vitakavyojengwa eneo hilo kuhakikisha vinakuwa rafiki kwa makundi yote wakiwemo mama ntilie, baba ntilie na waendesha bodaboda ili makundi yote yaliyokuwa yanafanya biashara eneo kutoathiriwa na mpango huo mpya.
Alitoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na wafanyabiashara wa eneo la Dumila kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa vibanda hivyo na kuhakikisha msaada huo unawanufaisha wafanyabiashara halisi waliokuwa wanafanya shughuli zao katika eneo hilo, badala ya kuingiza watu wasiohusika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale, alimshukuru Rais Mgufuli kwa msaada wa Sh mil. 100 kwa ajili ya kuwajengea wafanyabiashara maeneo bora ya kufanyia biashara zao.
Alisema wameanza kulitekeleza agizo la Rais kwa kuwatambua wafanyabiashara wa eneo la Feli-Dumila, na watafanya kazi hiyo kwa umakini na haraka ili wananchi wanaohusika waanze kunufaika na msaada huo mapema.
Kwa upande wake Meneja Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Nkolante Ntije, alisema agizo la Rais pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara lililenga pia usalama wa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Alisema wanapendekeza vibanda hivyo kujengwa upande wa kushoto wa barabara ukitokea Dodoma kwenda Morogoro ili kupunguza watu kukatisha mara kwa mara barabarani.