26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Straika URA aitamani Yanga

lwassa*Ni yule aliyewaua kombe la  Mapinduzi

NA MICHAEL MAURUS, ZANZIBAR

STRAIKA hatari wa URA aliyeiliza Yanga na Mtibwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika juzi visiwani hapa, Peter Lwassa, amesema anatamani mno kuchezea klabu ya Yanga inayonolewa na Mholanzi, Hans Van De Pluijm.

Mganda huyo ameeleza wazi kuwa anatamani kucheza pamoja na kiungo machachari Mzimbabwe, Thabani Kamusoko na mshambuliaji, Donald Ngoma.

Lwassa ndiye aliyefunga bao la kusawazisha la URA katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Yanga Jumapili iliyopita, akifanya hivyo akitokea benchi kipindi cha pili na hivyo kupeleka kipute hicho kwenye mikwaju ya penalti na timu yake kuibuka kidedea kwa ushindi wa jumla wa 5-4.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, juzi aliendelea kufanya maajabu yake kwa kuifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu, ikiwa ni baada ya kuingia uwanjani kipindi cha pili na kuiwezesha timu yake hiyo kushinda mabao 3-1 na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

Mabao yake hayo aliyoyafunga kwa ustadi mkubwa, yaliwafanya hata mashabiki waliokuwa wakiishangilia Mtibwa Sugar kubadilika na kumpigia makofi kuonyesha jinsi walivyomkubali, zaidi ikiwa ni uwezo wake wa kukaa katika nafasi na shabaha.

Baada ya mchezo huo wa juzi, MTANZANIA lilimfuata mkali huyo kutaka kufahamu siri ya cheche zake hizo ambapo alisema: “Hakuna miujiza yoyote, ni umakini tu na uwezo wa kuusoma mchezo.

“Kwa kawaida ninapokuwa benchi, huwa ninawasoma mabeki wa timu pinzani jinsi wanavyocheza, lakini pia wanavyojipanga. Hii hunisaidia kufahamu nikiingia nikae wapi niweze kupewa pasi ambayo itaniwezesha kufunga. Huwa ninapenda sana kuanzia benchi na mara zote ninapoingia sikosi kufunga,” alisema.

Juu ya timu ambayo angetamani kuichezea hapa Tanzania alisema kuwa amevutiwa mno na uchezaji wa Yanga ambao staili yake ndiyo anayoipendelea akiamini iwapo atapata nafasi ya kujiunga nayo, timu pinzani zitakiona cha moto.

“Yanga inacheza vizuri sana, wana kasi na wanashambulia, ninapenda sana soka la kushambulia muda wote kwani ndilo linaloiwezesha timu kushinda. Kwa wachezaji walionao kama yule kiungo wao mwenye rasta (Kamusoko) na straika wao mrefu mwenye nguvu (Ngoma), nikipangwa nao nitafunga kila mchezo,” alisema.

Alipoulizwa juu ya Simba, alisema: “Simba nao ni wazuri, lakini wanapiga pasi nyingi sana ambazo hazina madhara kwa mpinzani, lakini pia wanaonekana kuwa na wachezaji wenye vipaji, ni timu nzuri.”

Lwassa ambaye huvaa jezi namba 10 katika kikosi cha URA, amesema kuwa timu yoyote ya Tanzania itakayomtaka, yupo huru kujiunga nayo japo angependelea zaidi kujiunga na Yanga.

Kikosi cha URA kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo kwenda Uganda, ikiwa ni baada ya kuonyesha kandanda la aina yake kwenye michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles